Mwalimu: Kapigeni kura mkifikiria mashimo mlioachiwa kwenye migodi yenu

Shinyanga. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia  Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, amewahimiza wakazi wa Shinyanga kujitokeza kupiga kura Oktoba 29, wakikumbuka mashimo yaliyosalia katika migodi yao.

Mwalimu ameyasema hayo leo, Alhamisi Oktoba 23, 2025, katika mikutano ya kampeni iliyofanyika kwa nyakati tofauti kwenye majimbo ya Msalala na Itwangi, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.

Amesema wananchi hao walikuwa na mgodi wa Bulyanhulu, akiwataka  kujiuliza kuwa mgodi huo umeacha alama gani, licha ya kuwa na rasilimali waliyopewa na Mungu.

“Dhahabu imechimbwa tani kwa tani, leo tunaulizana maisha ya watu wa Shinyanga hali  ikoje, ndio  maana Chaumma tumekuwa  tukisema kuwa wananchi waamke kwa kuwa hivi vitu sio vya kudumu, vitakapoisha tutakuwa wageni wa nani,” amesema Mwalimu na kuongeza kuwa;

“Nasisitiza hakuna soko la kuuza utajiri bali nchi kutumia rasilimali walizonazo kuwanufaisha wananchi na Mungu alituletea dhahabu alijua watu wa Msalala, Itwangwi ma Shinyanga kwa ujumla mtatajirika,” ameeleza.

Aliwauliza wakazi hao ni wangapi wanakumbuka malori yaliyokuwa yakisafirisha dhahabu kutoka eneo hilo, wakati wengine wakifurahia maisha, lakini leo wameachiwa mashimo huku maisha yao yakiwa hayajabadilika.

“Niambie maji safi na salama yaliyopo hapa, barabara nzuri inayowaunganisha na Kahama na Geita, nionyesheni ambayo madini yalichimbwa yakaleta hayo.

Amesema kutokana na changamoto hizo, moja ya mambo yaliyowekwa katika ilani yao ni kuhakikisha wazawa wanamiliki sehemu ya rasilimali zitakapochimbwa, ili uchumi na manufaa yake yabaki nchini Tanzania.

“Niwaulize leo mna nini cha kuwatambia watoto wenu kwamba hapa kuliwa na mgodi hapa na hata wale Wazungu walikuwa wakitua hapa na ndege kila saa  hawapo kwa sababu wamemaliza chao na ule uwanja wa ndege uliojengwa kwa ajili yao leo umejaa nyasi.

“Amkeni ndugu zangu, wamemaliza dhahabu hapa, watagundua kwingine, watamaliza na hakutakuwa na huduma za afya, barabara nzuri, ajira, tunabaki masikini,” amesema.

Katika sekta hiyo ya madini, Mwalimu alikumbushia aliyoyafanya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, akieleza kuwa alikuwa na maono, kwani hakuchimba dhahabu wala almasi za nchi hii, na alipoulizwa sababu, alisema Taifa lake halikuwa na uwezo wa kuchimba wakati huo.

Pamoja na maamuzi hayo, amesema Mwalimu Nyerere alijenga barabara kwa mapato ya mauzo ya pamba, kahawa na mkonge,  biashara ambazo pia ziliwezesha kuwainua Watanzania kiuchumi.

“Hakuchimba mafuta wala gesi, lakini chama tawala leo kinashindwa kuyafanya yote hayo licha ya kuwa wanachimba madini, gesi na mafuta yetu.

“Rasilimali hizi sio za kudumu zikitumika zinaisha na zikitumika vibaya zinatuacha na umasikini wetu,” amesema.

Awali, mgombea ubunge wa Msalala kupitia Chaumma, Furahisha Wambura, amesema jimbo hilo lenye kata 12 limebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi, ikiwemo madini, lakini linakabiliwa na migogoro mingi ya mikataba inayowabana wananchi.

“Kwa hiyo ukiwa rais tunaomba uone namna  gani  ya kutatua kero hiyo,” amesema Furahisha.

Amesema changamoto nyingine ni upatikanaji wa pembejeo, ambapo wananchi wanashindwa kumudu gharama kutokana na bei yake kuwa juu.

“Ukiacha hayo  pia tumekuwa wahanga wa miundombinu ya barabara zinazounganisha kata moja kwenda nyingine na endapo zikinyesha mvua huwezi kupita katika barabara hizo,” amesema.

Kwa upande wa afya, mgombea ubunge huyo amesema kuwa ingawa kata yao ina zahanati, kuna daktari mmoja tu, jambo linalosababisha changamoto katika utoaji huduma.

Pia, amesema zahanati hiyo haina dawa, hivyo wananchi wanapokwenda kupata huduma huandikiwa nakwenda kununua nje.

Kuhusu suala la maji, Furahisha amedai kupata huduma hiyo imekuwa kitendawili licha ya awali wananchi kuchanga Sh7 milioni kwa ajili ya kufikishiwa huduma hiyo.