Mwamuzi aliyefungiwa miezi mitatu na kumaliza adhabu, apewa onyo kali ZPL

UNAMKUMBUKA mwamuzi Thobias Wariko, aliyefungiwa kwa muda wa miezi mitatu kutokana na kushindwa kutafsiri vyema sheria za mpira wa miguu katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ZFF Cup) iliyomalizika kwa KVZ kuichapa Uhamiaji mabao 2-1, Juni 11, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja, kisha vurugu kubwa zikatokea, sasa amepewa onyo kali ikiwa ni baada ya kumaliza adhabu na kuendelea na majukumu yake.

Katika mechi hiyo ambapo baada ya mwamuzi kupuliza filimbi kuashiria mechi imemalizika, zilitokea vurugu ambapo baadaye klabu ya Uhamiaji ilitoa taarifa ikieleza wachezaji wake saba pamoja na baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi walijeruhiwa vibaya. Majeruhi hao walifikishwa katika Kituo cha Polisi Madema ambako walipewa PF3 kwa ajili ya kuanza mchakato wa matibabu.

Sasa baada ya kumaliza adhabu yake na kuchezesha mechi za Ligi Kuu Zanzibar msimu huu, amekutana na onyo kali kutoka Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya Bodi ya Ligi Zanzibar (ZLB).

Taarifa iliyotolewa Oktoba 22, 2025 na Ofisa Habari wa ZLB, Issa Chiwile, imesema kamati imempa onyo kali mwamuzi Thobias Wariko kwa kushindwa kusimamia vyema sheria 17 za Mpira wa Miguu na kumtaka kuwa makini wakati wote wa mchezo. Mwamuzi huyo alichezesha Mchezo nambari 29 kati ya Muembe Makumbi City dhidi ya Kipanga, Oktoba 17, 2025 kwenye Uwanja wa Mao B, Unguja na kumalizika timu hizo zikishindwa kufungana.

“Kamati imeifuta kadi ya njano aliyoonyeshwa mchezaji Mohamed Mussa wa Muembe Makumbi City ambayo hakustahiki kuonyeshwa kwa mujibu wa sheria 17 za Mpira wa Miguu, kadi hiyo imefutwa kwa mujibu wa Sura ya 7 kanuni ya 8 ya kanuni za Mashindano toleo la 2025/2026.

“Aidha kamati imempa onyo kali mwamuzi Thobias Wariko kwa kushindwa kusimamia vyema sheria 17 za Mpira wa Miguu na kumtaka kuwa makini wakati wote wa mchezo.”

Mbali na hilo, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya Bodi ya Ligi Zanzibar (ZLB) katika vikao vyake vya kawaida vilivyofanyika Oktoba 15 na 20 Oktoba, 2025, ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Mzunguko wa 3 na 4 ya Ligi Kuu ya Zanzibar msimu wa 2025-2026.

“Kamati imeitoza faini ya shilingi laki tano (Sh500,000) timu ya Polisi SC kwa kosa la mchezaji wa timu hiyo, Stivin Emanuel aliyevalia jezi nambari 6, kwenda kwenye goli ambalo linatumiwa na timu ya Mlandege na kurusha vitu mithili ya mchanga golini kitendo ambacho kinashabihiana na imani za kishirikina, adhabu hii imetolewa kwa mujibu wa Sura ya 30 kanuni 2, (i).

“Vilevile Kamati imetoza faini ya shilingi laki tano (Sh500,000) timu ya Polisi SC kwa kumtumia mtu ambaye hakuorodheshwa kwenye fomu ya uwanjani kuingia uwanjani na kusimamia mazoezi ya viungo ya wachezaji wa Polisi, adhabu hii imetolewa kwa mujibu wa Sura ya 17 kanuni 1,” imeeleza taarifa hiyo ya ZLB.

Taarifa hiyo imeendelea kwa kusema: “Mchezo nambari 29 kati ya Muembe Makumbi City dhidi ya Kipanga, Kamati imeitoza faini ya shilingi laki tano (Sh500,000) timu ya Kipanga kwa kosa la kutumia mlango wa upande wa mashariki ya Uwanja wa MAO, mlango ambao si rasmi kutumika na klabu kwa kuingia uwanjani, kitendo ambacho ni kinyume na utaratibu na kinashabihiana na imani za kishirikina, hivyo ni kosa kwa mujibu wa Sura ya 30 kanuni ya 1 ya kanuni ya mashindano toleo la 2025/2026. Adhabu hio imetolewa kwa mujibu wa SURA ya 30 kanuni 2, (i),ya kanuni ya mashindano ya toleo la 2025/2026.”