OMO aahidi kujenga chuo kikuu cha Maalim Seif Pemba

Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Othman Masoud amesema atamuenzi Maalim Seif Sharif Hamad kwa namna anavyostahiki ikiwemo kujenga chuo kikuu cha mwanasiasa huyo, katika mji wa Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Maalim Seif ambaye alikuwa mwanasiasa mkongwe visiwani humo, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alifariki dunia Februari 17,2021 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ametoa ahadi hiyo leo Alhamisi Oktoba 23, 2025 katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika uwanja wa Jadida Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, uliohudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi.

Kabla ya kutoa ahadi kwenye mkutano huo wa kampeni, Othman amedai kuwa licha ya Maalim Seif kuwa na mchango mkubwa wa maendeleo visiwani humo, bado hajaenziwa inavyopaswa na watawala.

“Nashangaa viongozi wa Zanzibar, wameshindwa kumpa mtu huyu heshima (Maalim Seif) wamejenga shule, lakini wameshindwa hata kuzipa jina la Maalim Seif badala yake wanapewa wengine. Wameshindwa kumpa hata heshima.

“Niseme mbele yenu wananchi wa Wete na Wazanzibari kwa ujumla, nachukua jukumu na kutoa ahadi ya kumuenzi Maalim Seif kwa namna anayostahiki, miongoni hatua hizo ni kujenga chuo cikuu cha Maalim Seif hapa Wete,” amesema.

Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, amesema akishika madaraka Oktoba 29 ataitimiza ahadi hiyo, kwa sababu Maalim Seif ni mtu anayestahiki heshima zaidi.

Hata hivyo, ili kufanikisha ahadi hiyo mgombea huyo, amewaomba Wazanzibari kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, kumpigia kura yeye, wabunge, wawakilishi na madiwani.

Othman ametumia nafasi kuwatoa hofu Wazanzibari kutokuwa na wasiwasi kuhusu Oktoba 29, akiwataka kutuliza mioyo yao, kwa kila kitu kitakuwa sawa katika mchakato huo.

“Kuweni na amani, msiwe na wasiwasi jipangeni kwa ajili ya kupiga kura. Haya mengine tuachieni viongozi tutayaweka sawa, hakuna mchezo safari hii, hawa wameisha…niwaombe msibabaishe twendeni tukipige kura.

“Ahadi yangu ni kuifufua Wete ili uwe mji wa biashara kama zamani kupitia bandari mpya nitakayoijenga. Lazima tuirejeshe heshima ya Wete, kikubwa tukapige kura msitetereke hata kidogo,” amesisitiza Othman.

Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa amesema kuwa kisiwa hicho kimeiva kwa ajili ya mabadiliko yatakayofanywa na Wazanzibari watakaomchagua Othman Oktoba 29 awe Rais wao.

“Pemba inachemka, Unguja inachemka. Miaka ya hivi karibuni, baadhi ya mataifa yalifanya mabadiliko kwa kuwaondoa viongozi wa vyama tawala kupitia sanduku la kura.”

“Sasa basi upepo wa mabadiliko umehamia Zanzibar Oktoba 29, tunakwenda kuwafungasha virago na Othman Masoud anakuwa Rais wa Zanzibar,” amesema Jussa.

Katika mkutano huo, Jussa amewashukuru wananchi wa Wete kwa kujitokeza kwa wingi hatua walioifananisha na enzi za Maalim Seif Sharif Hamad (aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho), ambapo umati wa watu ulikuwa ukifurika katika mikutano yake.

Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma ACT Wazalendo, Salim Biman amesema zimebaki siku sita za kuondoa CCM katika sanduku la kura.

“Mwisho wa CCM umefika, wampishe Othman Masoud Othman aongoze Zanzibar,” amedai Biman.

Wakati Biman akieleza hayo, Naibu Katibu wa ACT-Wazalendo, Zanzibar Omar Ali Shehe amesema mkutano huo, ndio wa mwisho kwa Othman katika ratiba zake za mikutano ya majimbo.

“Hili ni jimbo la 18 kwa Pemba, tumekamilisha majimbo yote. Kwa mikutano 36 ya majimbo huu ndio wa mwisho na kwa majimbo 50 Zanzibar hili ndio jimbo la mwisho pia, piga makofi kwa Othman.

“Tunashukuru sana Mwenyekiti (Othman) kwa kufanya kazi nzuri ya kizalendo kwa ajili ya Wazanzibari kukupeleka Ikulu. Pia, tunakushuru Mwenyekiti wa timu ya ushindi ACT, Ismail Jussa,” amesema Shehe.