Pointi nne zampa mzuka Kocha Fountain Gate

KOCHA wa Fountain Gate, Mohamed Ismail ‘Laizer’ amesema kupata pointi nne kati ya sita katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara na kikosi hicho, zimeamsha morali kubwa kwa wachezaji kupambana zaidi, baada ya kuanza vibaya tangu msimu umeanza.

Kauli ya kocha huyo inajiri baada ya timu hiyo kulazimishwa sare juzi ya bao 1-1 dhidi ya Coastal Union, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, ikiwa ni mwendelezo mzuri baada ya ushindi wa 1-0 mbele ya Dodoma Jiji.

“Sio rahisi kupata pointi nne kati ya sita ambazo tulitakiwa kuzipata, baada ya kuanza vibaya nilikaa na wachezaji na kuwaeleza huu ni mwanzo tu na tuna muda wa kurekebisha hali iliyopo, nashuruku wanaanza kunielewa taratibu,” amesema.

Laizer amesema unapopoteza mechi mfululizo huwa inashusha morali ya wachezaji kijumla na inachukuwa muda kuirejesha, ingawa matokeo mazuri ya siku za hivi karibuni yanatoa mwanga mzuri, hasa baada ya nyota wapya kuanza kucheza kikosini.

“Hata ushindani wa mchezaji mmoja na mwingine unaongezeka jambo ambalo kwetu kama benchi la ufundi linatupa morali ya kufanya machaguo zaidi kikosini, bado tuna safari ndefu lakini kwa mechi mbili zilizopita zimetuongezea motisha zaidi,” amesema.

FOU 01
FOU 01

Mechi hiyo ya Coastal Union, ni ya tatu kwa Laizer kuiongoza Fountain Gate tangu arithi mikoba ya Denis Kitambi, ambaye aliondoka kwa makubaliano ya pande mbili na alianza kwa kichapo cha mabao 2-0, dhidi ya Mtibwa Sugar, Septemba 28, 2025. 

Laizer akashinda mechi ya kwanza msimu huu kwa kuifunga Dodoma Jiji kwa bao 1-0, Oktoba 17, 2025, kisha sare ya 1-1 na Coastal Union Oktoba 22, 2025, huku miwili ya Denis Kitambi alipoteza kwa kuchapwa 1-0, dhidi ya Mbeya City, Septemba 18, 2025.

Mechi ya mwisho kwa Kitambi, ilikuwa ya kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Simba, Septemba 25, 2025, huku Laizer ambaye kwa msimu wa 2024-2025, akikumbukwa zaidi ndani ya kikosi hicho cha Fountain Gate, baada ya kukinusuru pia kutoshuka daraja.