Profesa Mkenda amwombea kura Rais Samia akisema ameleta mageuzi makubwa ya elimu nchini

Rombo. Mgombea ubunge wa Jimbo la Rombo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Profesa Adolf Mkenda, amesema kuwa mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, anastahili kuendelea kuiongoza nchi kutokana na mafanikio na mageuzi makubwa anayoyaendeleza katika sekta ya elimu nchini.

Akizungumza leo Oktoba 23, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Zahanati ya Msangai, Kata ya Nanjara, Profesa Mkenda amesema sekta ya elimu imepata msukumo mpya chini ya uongozi wa Rais Samia kupitia miradi mbalimbali ya miundombinu, upanuzi wa fursa za elimu ya juu na maboresho ya huduma za elimu kote nchini.

“Rais Samia ameonyesha dhamira ya kweli kubadilisha mfumo wa elimu nchini,  tumeona mageuzi makubwa ya elimu hapa nchini,  shule nyingi zikijengwa, mabweni mapya kujengwa na programu mbalimbali zinazolenga kuinua kiwango cha elimu kwa watoto wetu,” amesema Profesa Mkenda.

Amesema kuwa, kupitia uongozi wa Rais Samia, fedha nyingi zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Jimbo la Rombo.

“Hapa jimboni tumefanikiwa kuongeza idadi ya shule za sekondari kutoka 41 hadi 46, tumejenga chuo cha VETA cha Serikali na sekondari ya ufundi ili watoto wetu wapate elimu itakayowawezesha kujiajiri au kuajiriwa kwa urahisi,” amesema Profesa Mkenda.

Profesa Mkenda, amesema kuwa mageuzi yanayoendelea katika elimu ni makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1967 wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, hayati Julius Kambarage Nyerere, aliyebadilisha mfumo wa elimu wa wakati huo.

“Sasa hivi chini ya Rais Samia, mageuzi mengine makubwa yanafanyika, baada ya elimu ya lazima kufikia darasa la saba, ifikapo mwaka 2027 kila mtoto wa Kitanzania atalazimika kusoma hadi kidato cha nne, hii ni hatua kubwa sana katika historia ya elimu nchini,” amesema Profesa Mkenda.

Kutokana na mafanikio hayo makubwa amewaomba  wananchi wa Jimbo hilo  kumuunga mkono na kumchagua mgombea urais huyo  kuendelea kuongoza katika nafasi hiyo ya urais katika uchaguzi mkuu unaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Mgombea udiwani wa Kata ya Nanjara, Joseph Masika amesema endapo atachaguliwa kuwa diwani wa kata hiyo atahakikisha anashirikiana na Serikali kukamilisha ujenzi wa barabara ya Kasirwa, ambayo imekuwa ni changamoto kupitika wakati wa kipindi cha mvua.