Dar es Salaam. Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameeleza namna Serikali yake ilivyojipanga kuijenga Tanzania jumuishi huku akiwataka vijana nchini wasidanganyike kuharibu amani na utulivu.
Samia amesema hayo leo Alhamisi Oktoba 23,2025 wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Tanesco Buza, Temeke jijini Dar es Salaam.
Samia amewahakikishia vijana kuwa, hakuna mwenye hati miliki ya nchi bali ni ya Watanzania wote.
“Nataka kuwahakikisha vijana wa Tanzania, msidanganywe… mkichukua Afrika Mashariki, Kusini na Kati, Tanzania ni pepo mko kwenye nchi yenye jina, kuendeleza watu wake. Msidanganywe na wale waliopo nje, huko asiwadanganye hapa mko pazuri kwelikweli, mkipata fursa ya kuingia kwa majirani zetu hapo muone vijana wenzenu wanavyokula ngumu, unaweza ukasema narudi Tanzania ndiyo kwetu,”amesema Samia.
Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan
“Niwaambie vijana, sisi wazazi wenu tunapita, nchi hii inawategemea ninyi tunatarajia tuwaachie nchi muiendeshe kama tunavyoendesha. Msidanganywe hata kidogo na katika kuendesha nchi kuna mfumo mzuri sana ambao kila baada ya miaka mitano tunachaguana nani atuendeshe, nani ashike nafasi gani katika ngazi tofauti.
“Wanangu, niwaombe sana vijana wa Kitanzania… Kaeni vizuri, nchi hii ni yenu, ni mali yenu, si mali ya mwingine … hakuna mwenye ‘certificate’ anayesema hii nchi ni mali yake, wengine wanasema sisi tunawakilisha wananchi, wananchi ni ninyi hapo na wengine hakuna mwenye milki ya wananchi.
“Tunapeana majukumu, niwaombe sana msiharibu nchi yenu wala amani ya nchi yenu, fuateni Serikali yenu inavyowaelekeza, Katiba na sheria za nchi zinavyoelekeza na mtaishi kwa salama na amani,” amesema mgombea huyo.
Samia amesema waasisi wa Taifa akiwamo hayati Mwalimu Julius Nyerere, alieleza ili nchi ipate maendeleo lazima iwe na watu, ardhi, siasa safi na uongizi bora.
“Tumekuwa tukiyaimba haya na kufanyia kazi na CCM imeamua kwenye ilani iliyopita, na ilani tunayoenda kutekeleza tujikite kwenye watu, tuendeleze watu, tuendelee kujenga na kuheshimisha utu wa Mtanzania,” amesema Samia.
Akizungumzia uchumi, amesema kwenye eneo hilo Serikali imefanya kazi nzuri na kujenga uchumi, kuanzia uchumi mkubwa hadi mdogo pamoja na kutoa fursa na maeneo ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo.
Kuhusu haki, amesema wameimarisha mhimili wa Mahakama na kwa sasa, haki zinapatikana kwa wakati.
“Kuhusu uhuru wa mtu kama ilivyo kwenye Katiba, kusema na uhuru usiokwenda kinyume na mila na desturi zetu na utu wa Mtanzania unasimama vema,” amesema na kuongeza;
“Zamani watu walipenda kujiita sisi wanyonge na walikuwa wanyonge ila kwa sasa ni tofauti. Kwenye ardhi tuna ardhi kubwa ila tulikuwa na kasoro ya upangiliaji, hatukufanya haki kugawanya ardhi ila CCM imejipanga vema kutumia ardhi kuzalisha na kufanya mambo mengine,” amesema Samia.
Akizungumzia siasa safi amesema ni ile inayohakikisha nchi iko salama, watu wanajumuishwa kufanya uamuzi wa mambo yao kupitia kamati na tume mbalimbali zinazohakikisha nchi iko salama na watu wako salama.
“Hata yanapotokea mazonge, tunazungumza na watu wanatoa maoni yao ili kuhakikisha siasa safi, mnafokeana na kuudhiana mnaitana na kuzungumza. Hayo ni mambo Nyerere alituambia na serikali zetu zimekuwa zikitekeleza haya kwa viwango tofauti,” amesema.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Thabit Kombo ameeleza namna ufunguaji wa nchi ulikuwa moja ya agenda kuu za Samia, akisema vijana wa Kitanzania wenye umri kati ya miaka 20 hadi 35 watapata ajira nchi za nje kupitia mikata ambayo Tanzania imeingia.
Amesema moja ya maeneo ambayo Samia ataendelea kuweka historia ni uzalishaji wa ajira kwa vijana.
Kombo amesema pamoja na kwamba Serikali imetoa ajira nyingi kwa Watanzania, sasa fursa hiyo imeenda hadi nje ya mipaka ya Tanzania.
“Tayari tumeingia mkataba na nchi za nje, vijana wa Kitanzania 50,000 wanaenda kupata ajira. Tutaenda kuhakikisha vijana hawa watafanya usaili na kufaulu ili idadi hiyo itimie,” amesema na kumkabidhi Samia mkataba huo (hakutaja nchi gani wamekubaliana nayo).
“Umezalisha ajira ndani ya nchi na sasa umezalisha fursa nje ya nchi. Kuna ajira nyingine 20,000 tunatarajia kuingia makubaliano na nchi nyingine. Vijana wetu sasa wakae mkao wa tayari kwa ajili ya fursa hizi,”amesema Kombo.
Waziri huyo amesema jitihada hizo zilikuwa ni moja ya mchango wa wizara hiyo kwa Samia kutokana na uboreshaji wa mashirikiano na mataifa mengine.
Mmoja wa waratibu wa kampeni za CCM mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda amesema umoja huo ulijipanga kufikia wanawake milioni 16.7 ila hadi sasa wamefikia wanawake milioni 15.7 kuhamasisha wamchague Samia.
“Nimetumwa na wanawake Tanzania, wako tayari kuhakikisha unashinda kwa kura za kishindo, wanawake hasa sisi wa UWT toka ulipotangazwa kuwa mgombea, tulianza kuweka mikakati kuhakikisha tunakuheshimisha na usiogope wanawake wenzio tupo na ni wapigakura wazuri, hata wasemeje umefanya kazi nzuri kwa miaka minne lazima tukuheshimishe,” amesema Chatanda.
Kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa amesema Watanzania wana sababu za kumchagua Samia kutokana na yale aliyotekeleza katika kipindi cha uongozi wake ikiwamo kampeni ya msaada wa kisheria ya Samia Legal Aid.
Msingwa amesema vyama vya upinzani kwa miaka 30 vimeshindwa kuja na sera mbadala dhidi ya sera za CCM na kuwa ilani ya chama hicho ya 2020/25 na ilani mpya inayotarajiwa kutekelezwa 2025/30 zinajali wananchi wa Tanzania.
“Ilani ya CCM pekee inashughulika na kahawa, korosho, pamba na alizeti za Watanzania. Nimekuwa upinzani zaidi ya miaka 20 lakini toka mfumo wa vyama vingi uanze vyama vyote vya upinzani Tanzania vimeshindwa kutoa sera mbadala za afya, kilimo au za kukuza uchumi dhidi ya CCM,” amesema.
“Samia aliona Watanzania ambao hawawezi kumudu gharama za mawakili, watu wengi hasa vijijini wanahangaika na ardhi, wana shida zinazohitaji msaada wa kisheria ndiyo maana kupitia kampeni ile aligusa wananchi zaidi ya mikoa 15.
“Tanzania yetu ni nzuri hatuhitaji kuichoma moto nchi yetu kwa hamasa ambazo hazina sababu, hii ndiyo nyumba yetu. Maamuzi ya hasira au jazba hayawezi kutusaidia hata marais waliopita hawakumaliza yote walifanya kwa kiasi na Samia alifanya pia kwa wakati wake,” amesema.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Ziwa Victoria, Ezekiah Wenje amesema kususia uchaguzi siyo suluhisho la changamoto katika jamii.
Hata hivyo, amewataka wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kutosikiliza propaganda mbalimbali zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii.
“Kuna maisha baada ya siasa, siasa siyo ugomvi, tunakuja kwa wananchi kuuza sera, kule majirani wana kiburi, wanaamini wanaungwa mkono na wananchi, hivyo wanaweza kufanya lolote. Mwaka 1995 alikuwepo Augustino Mrema akiwa NCCR- Mageuzi, leo NCCR iko wapi?,” amehoji.
“Kule Zanzibar kulikuwa na Chama cha CUF, leo siamini CUF kama wanapata viti vitano Pemba, haya majira kama wanachukulia for granted, kwamba wananchi wanawaunga mkono na ndiyo maana wamesusia uchaguzi…”
“Asilimia 80 ya Dar es Salaam (watu) wako kwenye mitandao ya kijamii, ninyi ndiyo walaji wa propaganda nyingi kupitia mitandao ya kijamii,” amesema Wenje.
