Dar es Salaam. Serikali imeanza kuchukua hatua mpya ya kuhakikisha kila mfanyakazi nchini anafanya kazi katika mazingira salama, kwa kushirikiana moja kwa moja na vyama vya wafanyakazi.
Hatua hiyo inalenga kupunguza ajali na magonjwa yanayotokana na kazi.
Katika mkakati huo, Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha) umeanza kutoa mafunzo maalumu kwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini, wakianza na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (Tughe) mkoa wa Dar es Salaam.
Zaidi ya viongozi 180 wa chama hicho, wakiwemo wenyeviti na makatibu wa matawi 90, wamepatiwa mafunzo ya awali kuhusu namna ya kuboresha mazingira ya kazi, katika kikao kazi kilichofanyika kwa siku mbili mjini Kibaha, mkoani Pwani.
Mtendaji Mkuu wa Osha, Khadija Mwenda, leo Oktoba 23,2025 jijini Dar es Salaam amesema mafunzo hayo ni mwanzo wa ushirikiano mpana zaidi kati ya Serikali na vyama vya wafanyakazi, lengo likiwa ni kuwafikia wafanyakazi wengi zaidi kupitia viongozi wao wa vyama.
“Viongozi hawa ni kiungo muhimu kati ya Serikali, waajiri na wafanyakazi. Tukiwapa uelewa sahihi kuhusu usalama na afya, watakuwa mabalozi wazuri wa kuboresha mazingira ya kazi katika taasisi zao,” amesema Mwenda.

Ameeleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha masuala ya usalama na afya yanapewa uzito unaostahili, na sasa yanazingatiwa hata katika ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Tume ya Utumishi wa Umma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tughe Mkoa wa Dar es Salaam, Brendan Maro amesema ushirikiano huo ni ushahidi wa dhamira ya kweli ya Serikali kulinda ustawi wa watumishi wake.
“Osha ni mdau wetu muhimu, mafunzo haya yatasaidia viongozi wetu kuwaelimisha wanachama na kuimarisha usalama kazini, mfanyakazi akiwa na afya njema, tija inaongezeka,” amesema Maro.
Washiriki wa mafunzo hayo wamesema wamefungua ukurasa mpya wa uelewa kuhusu namna bora ya kujilinda na kuwalinda wenzao kazini.
“Tumejifunza kuwa afya na usalama si jukumu la mwajiri pekee, bali ni wajibu wa kila mfanyakazi,” amesema Norbetha Sanga, Katibu wa Tughe Tawi la Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA).
Simon Lwaho kutoka Osha, amesisitiza washiriki kuwahamasisha wafanyakazi wenzao sehemu za kazi kujifunza kanuni bora za usalama na afya kutegemeana na shughuli zao za kila siku, ili kupata mbinu za kujilinda dhidi ya vihatarishi mbalimbali vya magonjwa na ajali.