Sh12 bilioni zatengwa kulinda bayoanwai kwenye misitu nchini

Dar es Salaam. Jumla ya Dola za Marekani milioni 4.94  ambazo ni zaidi ya Sh12 bilioni, zimetengwa kufanikisha mradi jumuishi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda bayoanwai.

Mradi huo unakwenda kupunguza ukataji na uharibifu wa misitu, kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia na kuimarisha matumizi ya nishati safi katika shughuli za utalii ikiwamo usafiri wa e-mobility.

Kamishna wa Uhifadhi, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo amebainisha hayo leo Oktoba 23, 2025 katika uzinduzi wa kikao kazi cha utekelezaji wa mradi huo.

Amesema mradi huo utatekelezwa katika misitu minne ya Hifadhi za Mazingira Asilia.

Misitu hiyo ni Amani (Muheza), Magamba (Lushoto) na Nilo (Korogwe) iliyopo mkoani Tanga na Hifadhi ya Chome (Same) katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Profesa Silayo amesema maandalizi ya mradi yalianza miaka minne iliyopita yakifanyika kwa ushirikiano wa karibu kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais, TFS na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

“Hatua tuliyofika leo ni muhimu kwa ajili ya kuhakiki na kufanya mapitio muhimu ya kitaalamu kwenye andiko la mradi ili kuhakikisha mradi unatekelezeka ipasavyo na kuleta matokeo yaliyokusudiwa,” amesema.

Mradi huo unaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani awamu ya nane (GEF-8) utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2025 – 2030 katika misitu hiyo minne ya Hifadhi za Mazingira Asilia.

Profesa Silayo amesema mradi huo una thamani ya dola 4.94 milioni, kati ya fedha hizo, GEF watatoa dola 4.74 milioni na UNDP watachangia dola 200,000.

“Aidha, Serikali itachangia dola 29.3 milioni na wadau wengine watachangia dola 3.72 milioni kupitia miradi na shughuli za uhifadhi zinazotekelezwa katika maeneo ya mradi,” amesema. 

Akifungua kikao kazi cha kamati ya utekelezaji wa mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbas amesema mradi umekuja wakati sahihi ambao dunia inakabiliana na changamoto nyingi ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa gesijoto duniani.

“Ikumbukwe kuwa mchango wa misitu ni mkubwa katika kuhakikisha changamoto inapungua na kuendelea kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi,” amesema akifafanua kwamba mradi huo unaanzia kwenye mikoa ya Tanga na Kilimanjaro, kabla ya kwenda mikoa mingine hapo baadaye.

Amesema mradi huo ni kati ya miradi midogo 12 duniani (Country Net Zero Child Projects) katika Mradi Mkubwa wa Kidunia (Net Zero Nature Positive Accelerator Integrated Program – NZNP IP).

“Utekelezaji wa malengo ya mradi huu yanachangia katika mradi mkubwa wa kidunia, hivyo, tuna wajibu kuutekeleza vema kwani tusipofanya vizuri sisi tutakuwa tunakwamisha jitihada za wenzetu,” amesema.

Amesema jitihada za kutafuta fedha za utekelezaji miradi ya kimkakati zimefanya maeneo ya misitu nchini kuboreka na kuongeza mvuto wa kutembelewa na wageni, akitaja idadi ya watalii na mapato yameendelea kuongezeka katika eneo hilo.

Awali, Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini, Shigeki Komatsubara amesema mradi huu unakuja kipindi nyeti ambapo Tanzania inaendelea kutekeleza mkakati wa maendeleo wa muda mrefu wa uzalishaji mdogo wa hewa ukaa (LT-LEDS), na kuongeza kasi kuelekea kufikia uzalishaji sifuri wa hewa ukaa ifikapo mwaka 2050.

“Mradi wa hauhusu tu kupunguza uzalishaji wa gesi ukaa, bali unalenga kubadilisha namna tunavyosimamia misitu yetu, mifumo ya nishati, na ustawi wa jamii kwa ujumla,” amesema.

 “UNDP imeweka kipaumbele cha juu katika usimamizi endelevu wa rasilimali asili, ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, kupunguza athari za majanga, na mabadiliko kuelekea nishati jadidifu,” amesema.

Amesema mradi utasaidia malengo ya urejeshaji na usimamizi endelevu wa misitu, upanuzi wa soko la nishati safi na matumizi ya magari ya umeme (e-mobility) katika utalii.

Nje ya kikao kazi hicho, mtaalamu wa mazingira na usimamizi wa rasilimali asilia wa UNDP Tanzania, Gertrude Lyatuu, alisema mradi huo utahamasisha matumizi ya teknolojia safi za nishati katika maeneo ya hifadhi na misitu.

“Utazingatia zaidi uhifadhi wa misitu na kukuza matumizi ya nishati safi, hasa kwa kubadili magari ya kitalii kutoka yanayotumia dizeli kwenda yanayotumia umeme,” amesema Lyatuu.