TRC yataja chanzo ajali treni ya mchongoko, yachunguza

Dar es Salaam. Treni ya Electric Multiple Unit – EMU maarufu treni ya mchongoko iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Dodoma leo Alhamisi Oktoba 23, 2025 imepata ajali katika kituo cha Ruvu mkoani Pwani.

Hii ni ajali ya kwanza kutokea tangu kuanza kwa huduma ya reli ya kisasa nchini Tanzania.

Taarifa iliyotolewa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) imetaja chanzo cha awali cha ajali hiyo, huku ikieleza jitihada zinazofanyika sasa kuhakikisha huduma zinarejea.

“Shirika la Reli Tanzania (TRC) linautaarifu umma kuhusu ajali ya treni ya EMU iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma iliyotokea saa 2:00 asubuhi Oktoba 23, 2025 kutokana na hitilafu za kiuendeshaji, tukio hili limetokea kituo cha Ruvu na kwa taarifa za awali hakuna kifo.”

“Timu ya wataalamu ikiongozwa na Katibu Mkuu Uchukuzi, Mkurugenzi Mkuu TRC, vyombo vya ulinzi na usalama na menejimenti ya TRC inaendelea na uchunguzi wa kina na juhudi za kuhakikisha kwamba huduma zetu zinarejea haraka,” ilieleza taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa.

Picha mnato na mjongeo zimesambaa katika makundi sogozi ya Whatsapp zikionyesha hali halisi ilivyo.

Treni ya mchongoko, ambayo imekuwa ikifanya safari zake kutoka Dar es Salaam, Morogoro hadi Dodoma ilianza kutoa huduma Novemba Mosi, mwaka 2024.

Treni aina ya EMU imeelezwa kuwa ina uwezo wa kuchukua abiria zaidi ya 589 na inaweza kufikia kasi ya hadi takriban kilomita 160 kwa saa.

Mradi huu ulilenga kuboresha usafiri wa abiria na mizigo, kuongeza kasi, usalama, na pia kuunganisha Tanzania na mitandao ya reli za kanda ya Afrika Mashariki.

Tanzania Standard Gauge Railway (SGR) nchini Tanzania ilianza rasmi kusafirisha abiria kati ya Dar es Salaam na Morogoro Juni 14, 2024. Kisha safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma ilizinduliwa rasmi Julai 25 2024.