Arusha. Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amewataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wanachama wote kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa kuwachagua viongozi watakaosimamia na kutetea haki pamoja na maslahi ya wafanyakazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo Alhamisi, Oktoba 23, 2025, Nyamhokya amesema upo umuhimu wa wafanyakazi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kupiga kura na kuchangia katika kujenga taifa lenye uongozi unaojali maslahi ya watumishi wa umma na sekta binafsi.
“Tukumbuke kaulimbiu yetu ya Mei Mosi inasema: ‘Uchaguzi Mkuu wa 2025 utuletee viongozi wanaojali haki na maslahi ya wafanyakazi’, hii haiji kwa kulala nyumbani hivyo tujitokeze kwa wingi tushiriki katika uchaguzi huu kwa kuwachagua viongozi wenye dhamira njema na wanaosimama kidete kutetea haki za wafanyakazi,” amesema.
Amesema hadi sasa wafanyakazi wote wako salama na nchi nzima iko salama, hivyo hakuna sababu ya kukaa nyumbani siku hiyo muhimu ambayo itakuwa na mapumziko.
“Niwaombe wafanyakazi wote Oktoba 29 msilale nyumbani. Nendeni mkapige kura na kisha muendelee na shughuli zingine kwani, siku hiyo itakuwa ya mapumziko. Tukitumie ipasavyo kwa kufanya maamuzi sahihi kwa mustakabali wa taifa letu.
“Kubwa ni kuhakikisha unamchagua kiongozi ambaye ukienda kumweleza jambo au changamoto yoyote atakusikiliza na kuchukua hatua. Tunahitaji viongozi wanaoheshimu sauti ya wafanyakazi na walio tayari kushirikiana nasi katika kuboresha mazingira ya kazi na ustawi wa wananchi,” amesema Nyamhokya.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Tucta, Hery Mkunda amesema wao kama vyama vya wafanyakazi wako tayari kushiriki uchaguzi mkuu ujao kwa maslahi na hatma njema ya wafanyakazi.
“Ninachoomba viongozi wa vyama na wanachama wahakikishe hawawi chanzo cha kuzuia kwa namna yoyote mchakato wa uchaguzi bali wanakuwa mfano wa kushiriki kwani, hatma ya changamoto zetu ziko mikononi mwetu katika kubakisha amani na utulivu uliopo.
“Kikubwa niombe ambao wanahamasisha watu wasishiriki uchaguzi waache kufanya hivyo bali watumie nguvu hiyo kuchagua yule ambaye wanaona anafaa kwa maslahi mapana ya Taifa,” amesema.
Naye Katibu wa Chama cha waajiriwa wa Makampuni Binafsi Kanda ya Kaskazini (TUPSE), Aisha Masoud amesema wanaendelea kufanya hamasa kwa wanachama wao kuhakikisha wanajitokeza kupiga kura hasa kwa wale wanaoona wana uwezo wa kuwasemea katika maslahi yao.
“Sisi tunataka kiongozi ambaye atalinda, kusikiliza na kutetea maslahi yetu hivyo, tutajitokeza kwa wingi kuhakikisha tunachagua viongozi watakaotufaa bila kuangalia chama, jinsia wala umri,” amesema.