Tucta kusimamia utekelezaji wa nyongeza ya kima cha chini kwa sekta binafsi

Dar es Salaam. Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limeishukuru Serikali kwa kuifanyia kazi kwa vitendo hoja ya nyongeza ya mishahara kwa sekta binafsi kwa  kupandisha kima cha chini kwa asilimia 34.4 kutoka Sh275,060 hadi Sh358,322 kwa mwezi kitakachoanza kutumika Januari  1,2026.

Nyongeza hiyo ilitolewa kupitia Tangazo la Serikali Namba 605A la Tarehe 13 Oktoba 2025 ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu lililotolewa Oktoba 17, 2025.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari leo Oktoba 23, 2025 rais wa shirikisho hilo, Tumaini Nyamhokya amesema hoja hiyo ilikuwa kilio cha muda mrefu kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na kukiri kuwa, ofisi yake ilipata kiwango cha juu cha ushirikishwaji katika suala hilo.

Amesema Tucta ilishiriki katika bodi ya kima cha chini na ilipata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa kamati maalumu ya wataalamu ya iliyoundwa na Serikali ya kufanya utafiti kuhusu viwango vya kima cha chini cha mshahara wa sekta binafsi, mapendekezo yaliwasilishwa na kupokewa na Serikali.

Amesema shirikisho hilo litasimamia kikamilifu utekelezaji wa nyongoza hiyo na kuwataka wadau kutekeleza amri hiyo.

“Niendelee kutoa rai kwa waajiri ambao naamini sisi sote hapa tuna watu tumewaajiri sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na majumbani kuhakikisha kuwa, tunatekeleza amri hii kwa jumla. Tucta kwa kushirikiana na wadau wa utatu yaani Serikali na Chama cha Waajiri (ATE) tutaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa suala hili muhimu,”amesema Nyamhokya.

Mbali na nyongeza hiyo, amesema Serikali imefanya mambo kadhaa yenye tija kwa wafanyakazi wa umma na binafsi.

Amesema baadhi ya hayo ni  punguzo la kiwango cha makato kutoka asilimia tisa hadi nane kwa mishahara ya kima cha chini, kuongezeka kwa kasi ya kuidhinisha mikataba ya hali bora (CBAs) na mipango ya motisha kwa watumishi wa taasisi za umma na maboresho makubwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii yaliyowezesha kulipwa mafao ya wastaafu waliongoja kwa muda mrefu.

Mengine ni kuongezwa kwa umri wa mnufaika (mtoto) wa mwanachama wa NHIF kutoka miaka 18 ya awali hadi miaka 21, nyongeza ya siku za likizo kwa wafanyakazi wanaojifungua watoto njiti, kuongezeka kwa kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi na umma na kuondolewa kwa tozo ya asilimia sita kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

Mbali na hayo, katika kipindi hicho taasisi nyingi za umma zimeweza kuunda mabaraza ya wafanyakazi na kufanya vikao kwa mujibu wa sheria, Serikali kuendelea kuajiri watumishi wapya kwa wingi, hivyo kupunguza uhaba wa watumishi.

Sambamba na watumishi wa umma wapatao 412,530 waliopandishwa madaraja katika kipindi cha 2022-2024 huku kwa mwaka fedha 2024/2025 Serikali imetenga fedha za kuwezesha kupandishwa madaraja watumishi wapatao 219,042.

Katika kipindi hicho pia kima cha chini cha pensheni kimeongezwa kutoka Sh100, 000 hadi Sh150, 000 kwa mwezi na kuhuisha ongezeko la malipo ya pensheni ya kila mwezi kwa kiwango cha asilimia 2 kwa kuzingatia kanuni na sheria zilizopo kuanzia Januari 2025.