Vibali vya biashara kilio kipya kwa wafanyabiashara mipakani

Arusha. Vibali na vyeti vya biashara vimekuwa kilio kipya kwa wafanyabiashara wa mipakani katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wakilalamikia urasimu, gharama kubwa, na ukaguzi wa mara kwa mara unaochelewesha bidhaa kufika sokoni.

Sambamba na hilo vituo vingi vya ukaguzi wa mizigo barabarani husababisha hasara, hasa kwa bidhaa zinazoharibika haraka kama matunda na mbogamboga.

Kilio hicho kimewasilishwa leo Oktoba 23, 2025 kwenye mdahalo kati ya sekta ya umma na binafsi uliofanyika katika mpaka wa Namanga kuhusu vizuizi visivyo vya kodi (NTBs), uliowakutanisha wadau zaidi ya 70 wakiwemo wafanyabiashara wa mipakani, vyama vya mawakala wa forodha na mashirika ya uwezeshaji biashara.

“Upande wa Kenya kuna vituo vya ukaguzi barabarani zaidi ya vinane karibu kila kilomita chache na upande wa Tanzania vipo zaidi ya vitano, vingi vikiwa bila huduma za msingi,” amesema Naseriani Mosses, mfanyabiashara wa mazao.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Kimataifa la Usafirishaji na Uhifadhi wa Bidhaa (Kifwa), Alex Kabuga, amesema mchakato wa kupata vibali na cheti cha asili ni mrefu huku ukiwa na gharama kubwa.

“Pia, kuna tozo na gharama ambazo ni tofauti kati ya nchi wanachama, jambo linalosababisha kucheleweshwa kwa bidhaa na kupoteza faida.

 “Changamoto hizi zinakwamisha wafanyabiashara wadogo na kuathiri Mpango Rahisi wa Biashara (STR),” amesema.

Katika mdahalo huo ulioandaliwa na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) kwa kushirikiana na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na AGRA, ulilenga kubaini changamoto za wafanyabiashara wanawake na vijana mpakani na kutoa suluhisho la kuboresha biashara, ili kuwasaidia kuchangia katika ustahimilivu wa uchumi wa nchi zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa EABC, Adrian Raphael Njau ametumia nafasi hiyo kuitaka nchi za EAC kurahisisha utoaji wa vyeti na vibali, kupunguza gharama, na kuhakikisha mifumo ni sawa kanda kwa nzima.

Aliongeza kuwa hatua hii itaongeza ushindani, kurahisisha biashara, na kukuza uchumi wa kanda.

Mdahalo huo  ulienda sambamba na uzinduzi wa Kituo cha Taarifa za Biashara katika Kituo cha Pamoja cha Forodha (OSBP) Namanga, lengo likiwa ni kurahisisha upatikanaji wa taarifa, mwongozo wa STR, na taratibu za biashara.

Mtaalamu wa Vijana AGRA, Barbara Mbabazi amesema mdahalo huo uko chini ya mradi unaolenga kuwawezesha wanawake na vijana, kuboresha uelewa wao kuhusu taratibu za biashara na kuongeza uwezo wao wa kufanya biashara ya mahindi na mazao ya bustani katika mipaka ya EAC.

Mkurugenzi Mtendaji Mtendaji wa EABC, Adrian Raphael Njau akizungumza na wafanyabiashara wa mpaka wa Namanga kutoka Kenya na Tanzania

“Mpango huu ni sehemu ya mradi unaoendelea wa “Kukuza Biashara ya Kilimo na Chakula Ndani ya EAC kwa Kushughulikia Vikwazo Visivyo vya Kiforodha (NTBs),” amesema.

Amesema lengo ni kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara wanawake na vijana hasa katika sekta ya kilimo na chakula, kuchochea biashara ya mpakani ya mahindi, mchele, maharage, soya na mazao ya bustani katika njia kuu za biashara za EAC.

Mradi huu wa miaka mitatu (2024–2026), unaotekelezwa na EABC kwa usaidizi wa AGRA, unalenga kufikia takriban wafanyabiashara wanawake na vijana 2,440 katika ukanda mzima.

Mpango huu unafadhiliwa kwa ruzuku ya dola za Marekani 399,900 kutoka AGRA, kwa usaidizi wa ziada kutoka Mastercard Foundation na Bill & Melinda Gates Foundation (BMGF).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa EAC kutoka Tanzania, Amedeus Mzee, amesema kuwa mdahalo unalenga kukuza uchumi wa EAC kupitia utatuzi wa vikwazo visivyo vya kodi (NTBs) na maazimio yake yatawasilishwa katika mikutano ya viongozi wa juu wa nchi wanachama.