VYOMBO VYA HABARI VYAOMBWA KUWAPA WANAWAKE NAFASI SAWA KWENYE SIASA

:::::::::::::

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Muungano wa Asasi za Wanawake na Watetezi wa Usawa wa Kijinsia Tanzania umetaka vyombo vya habari kutoa nafasi sawa kwa wagombea wanawake kupitia midahalo, makala na vipindi vya mijadala vinavyolenga kuongeza uelewa wa umma juu ya uwezo na mchango wa wanawake katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mwanzilishi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Rose Haji, alisema asasi hizo zimeungana kuhimiza ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, sambamba na kuhamasisha wanawake kujitokeza kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu.

Bi. Haji alisema ushiriki wa wanawake katika siasa ni kipaumbele cha mashirika ya kiraia yanayolenga usawa wa kijinsia, akibainisha kuwa uwepo wa viongozi wanawake ni hatua muhimu katika kuinua kipato na kuboresha maisha ya wanawake nchini.

Aidha, alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika ajenda ya ushiriki wa wanawake kwenye siasa, akitaja mfano wa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea wengine wanawake wa urais kama Saumu Rashid (UDP) na Mwajuma Mirambo (UMD), hali inayodhihirisha ukuaji wa demokrasia.

Tamko hilo lilizitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na vyama vya siasa kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, salama na jumuishi, bila vitisho au ukatili wa kijinsia unaoweza kuwakatisha tamaa wanawake kushiriki.

“Asasi hizi zinatoa rai kwa wananchi kutohukumu viongozi wanawake kwa misingi ya jinsia bali kwa uwezo na dira yao ya maendeleo,” alisema Bi. Haji, akiongeza kuwa uongozi wa mwanamke ni chachu ya demokrasia jumuishi na maendeleo endelevu.

Alizitaka pia taasisi za habari nchini kuhakikisha zinatoa fursa sawa kwa wagombea wanawake kushiriki midahalo na mijadala ya kisera, akisisitiza kuwa “uongozi bora hauna jinsia bali unategemea maadili, dira na dhamira ya kuwahudumia wananchi wote kwa usawa.”