WANARIADHA sita walioiwakilisha Tanzania katika mbio za Nagai City Marathon zilizofanyika Japan, wamerejea nchini kwa furaha baada ya kufanya kweli.
Mbio hizo zilifanyika Oktoba 19, 2025 katika mji wa Nagai, ambapo Tanzania iling’ara katika mbio zote ambazo ilishiriki marathoni Kilomita 42 na nusu marathoni Kilomita 21, Wanaume na Wanawake.
Nyota hao walifanya kweli kwa kumaliza nafasi nne za juu, Kilomita 42 Wanaume, Michael Sanga akishika nafasi ya kwanza kwa muda wa 2:15:26, Charles Sulle akamaliza wa pili kwa 2:16:30 huku Vaileth Kidas kwa 2:41:37, upande wa Wanawake.
Kilomita 21, Joseph Panga alimaliza wa pili kwa 1:02:52 huku Jumanne Ndege akimaliza wa nne kwa 1:06:07, wakati Agnes Mwaghui akishinda kwa upande wa wanawake baada ya kutumia muda wa 1:12:51.

Akiwapokea wanariadha hao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Meja John Muna kwa niaba ya kamanda wa kikosi cha 833KJ, Jkt Oljoro amewapongeza wanariadha hao kwa juhudi kubwa ambazo wanaendelea kufanya kuhakikisha bendera ya nchi inapepea vyema Kimataifa.
“Sasa hivi imeonekana kuna mwendelezo mzuri kwenye riadha kama mwenzetu Simbu (Alphonce) alivyoonyesha kwa kushinda medali ya dhahabu katika mashindano ya riadha ya dunia na kuweka rekodi.
“Nawashukuru viongozi wangu wanatia hamasa katika mchezo huu na wachezaji muendelee kufanya mazoezi kwa bidii ili kufanya vizuri katika mashindano mengine,” amesema Muna.
Raisi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Rogath John Stephen Akhwari amesema wanariadha hao baada ya kufanya vizuri Nagai City Marathon watawahamasisha wenzao ambao ni chipukizi kufanya vizuri na kufikia mafanikio hayo.
Kocha wa timu ya riadha ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Mteule daraja la pili, Antony Mwingereza ameweka wazi kuwa wachezaji hao wameinyanyua taifa la Tanzania hivyo amewataka wengine nao kujituma kwa bidii katika kuiwakilisha nchi Kimataifa.

Nyota, Vaileth Kidas ambaye alishika nafasi ya kwanza Km 42, katika mbio hizo akizungumza kwa niaba ya wanariadha wenzake, amesema ushindani ulikuwa mkubwa ila nidhamu na bidii ambayo waliweka mbele ndio imekuwa siri ya mafanikio yao.
Wachezaji hao sita ambao walishiriki mbio za Nagai City, wawili walikuwa wanatokea Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), sawa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi mchezaji mmoja na raia mmoja.