Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv
ASASI za kiraia za wanawake zinazotetea haki na usawa wa kijinsia zimeitaka jamii na wadau wa siasa nchini kuhakikisha kipindi hiki cha kampeni na uchaguzi kinakuwa cha amani, heshima na hoja zenye kujenga taifa, badala ya kutumia lugha za kejeli, udhalilishaji au mashambulizi ya kibinafsi hasa kwa misingi ya kijinsia.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam leo Oktoba 23,2025 wakati wa kutoa tamko la Asasi za Wanawake kuelekea Uchaguzi Mkuu, wawakilishi wa mashirika hayo wamesema uchaguzi wa mwaka huu ni fursa ya kuimarisha demokrasia jumuishi na kuthibitisha kuwa uongozi bora hauna jinsia bali unaongozwa na maadili na dira ya maendeleo.
Mwandishi mkongwe na mmoja wa waanzilishi wa Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), Rose Mwalimu, amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG 5) kupitia uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo nchini.
“Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia mabadiliko ya sheria za kisiasa, utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo na kuongezeka kwa uwakilishi wa wanawake katika nafasi za maamuzi. Hii ni ishara ya taifa linaloamini katika usawa wa kijinsia,” amesema Rose
Amesema mwaka huu wagombea urais na wenza wanawake kutoka vyama mbalimbali ni ushahidi kwamba Tanzania inaendelea kusonga mbele katika kujenga siasa shirikishi na demokrasia ya kweli.
Aidha, Rose amesisitiza kuwa “uongozi wa mwanamke si tishio bali ni nyenzo ya kuimarisha demokrasia jumuishi yenye kusikiliza na kutenda kwa manufaa ya wote,” huku akitoa wito kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na vyama vya siasa kuhakikisha mazingira salama na huru dhidi ya ukatili wa kijinsia wakati wa uchaguzi.
Akirejea kauli ya Rais Samia aliyoitoa hivi karibuni kwenye mkutano wa kampeni jijini Dar es Salaam “Matusi niachieni mimi, ninayabeba kwa niaba yenu…” Mwalimu amesema ujumbe huo ni kielelezo cha uongozi wa hekima na ustahimilivu, unaostahili kuigwa na wanasiasa wote.
Kwa upande wake, Lucy Kilasi kutoka asasi ya Welfare Tanzania, ametoa wito kwa wanawake kuungana na kushirikiana zaidi badala ya kushindana, akisema mshikamano huo ni nguzo muhimu katika kufanikisha usawa wa kijinsia na maendeleo ya taifa.
“Ushiriki wa wanawake katika siasa ni chachu ya maendeleo. Wanawake viongozi mara nyingi hupigania elimu bora, afya, na haki za kijamii mambo ambayo yanagusa maisha ya kila Mtanzania,” amesema Lucy
Wadau hao wametaka vyombo vya habari kutoa nafasi sawa kwa wagombea wanawake katika mijadala, midahalo na makala za kisiasa ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu mchango wao katika ujenzi wa taifa.
“Taifa lenye usawa wa kijinsia ni taifa lenye amani, ustawi na maendeleo endelevu,” amesema Mwalimu akihitimisha.