𝗞𝗔𝗠𝗜𝗦𝗛𝗡𝗔 𝗔𝗜𝗣𝗢𝗡𝗚𝗘𝗭𝗔 𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗞𝗪𝗔 𝗨𝗔𝗗𝗜𝗟𝗜𝗙𝗨 𝗞𝗔𝗧𝗜𝗞𝗔 𝗨𝗧𝗨𝗠𝗜𝗦𝗛𝗜 𝗪𝗔 𝗨𝗠𝗠𝗔

Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kuendelea kuonesha uadilifu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yake ya kusimamia na kuhifadhi mazingira nchini.

Akizungumza leo 23 Oktoba, 2025 jijini Dar es Salaam katika ziara yake ya kikazi ofisi za Baraza Dkt. Laurean Ndumbaro amesema uadilifu uliooneshwa na Baraza hilo ni mfano wa kuigwa na Taasisi nyingine za Umma katika kuhakikisha huduma kwa wananchi zinatolewa kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili ya kazi.

Amesisitiza kuwa uadilifu ndio nguzo kuu ya utumishi wa umma na ndio msingi wa kuaminika kwa Serikali mbele ya wananchi.

Ameongeza kuwa mafanikio ya NEMC katika utekelezaji wa miradi ya kimazingira pamoja na usimamizi wa Sheria na Kanuni za Mazingira ni ushahidi kwamba viongozi na watumishi wake wameweka maslahi ya Taifa mbele kuliko maslahi binafsi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi amemshukuru Kamishna kwa Tathmini hiyo na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na ubunifu zaidi kwani pongezi hizo ni chachu ya kuongeza ari ya watumishi kulinda rasilimali za Taifa na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Katika ziara yake Kamishna Dkt. Ndumbaro ameambatana na wataalamu wengine akiwemo Mkurugenzi wa Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti kutoka Tume ya Utumishi wa Umma Ndugu Peleleja Masesa.