KATIBU Mtendaji Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar, Said Kassim Marine, amesema milango ya mchezo wa masumbwi visiwani hapa imefunguka kimataifa, hivyo wanamichezo wanapaswa kuitumia fursa hiyo ipasavyo.
Ameyasema hayo jana Oktoba 23, 2025 wakati wa kuwapokea mabondia, Ali Mkojani na Suleiman Mtumwa.
Mabondia hao walikwenda Brazil kushindana ambapo Mkojani amerejea na medali ya shaba baada ya kumaliza nafasi ya tatu.
Katika mapokezi hayo yaliyojaa mbwembwe nyingi, katibu huyo amesema, vijana hao wameshakuwa mabalozi wa kuitangaza Zanzibar kimataifa na wengine wanasisitizwa kufuata nyayo hizo kwa lengo la kuboresha sekta ya mchezo huo.
Naye Bondia wa ngumi za kulipwa Zanzibar, Ali Mkojani amesema wameonesha uwezo wa kutosha kuhakikisha wanaliwakilisha Taifa na hatimaye wamerudi na zawadi ya kumpatia Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.
Amesema, mapambano hayakuwa magumu sana kwani ni mchezo waliouziea lakini tatizo ni katika changamoto ya hali ya hewa iliyopo nchini humo.
“Pambano halikuwa gumu sana badala yake ni changamoto ilikuwa unapofika sehemu unapaswa kupumzika ili uzoee mazingira na hali ya hewa ya nchini humo,” amesema Mkojani.
Hatahivyo, ametoa wito kwa serikali kuupa kipaumbele mchezo huo kwa sababu unatengeneza ajira nyingi kwa vijana na Wazanzibar wanayo nafasi ya kushiriki mchezo huo duniani.
Bondia Suleiman Mtumwa, amesema licha ya wapinzani wao kujiandaa na mchezo huo, pia wao wamepata nafasi nzuri ya kuonesha vipaji vyao na wamefanikiwa kurudi na zawadi hiyo.
Bondia wa ngumi za kulipwa kutoka Zanzibar, Ali Mkojani aliwasili jana usiku Oktoba 23, 2025 akitokea jijini Rio De Jeneiro nchini Brazil aliposhiriki michuano ya ngumi ngazi ya klabu duniani, World Interclub Boxing Championship (WIBC).
Mashindano hayo, yalianza Oktoba 15, 2025 na kutamatika Oktoba 20, 2025 ambapo Mkojani amefanikiwa kutwaa medali ya shaba baada ya kushika nafasi ya tatu kwenye uzito wa Super Welter.
