Mara. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mara kimeungana na familia ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche na kutoa wito kwa Jeshi la Polisi kujitokeza hadharani na kutoa taarifa kuhusu alipo kiongozi huyo.
Aidha, chama kimewahimiza viongozi wa dini na wanaharakati wa haki za binadamu kupaza sauti kuhusu suala hilo.
Heche alikamatwa Oktoba 22, 2025 asubuhi katika viunga vya Mahakama Kuu ya Dar es Salaam alipokwenda kusikiliza kesi inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu na nyingine ya raslimali za chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa leo Oktoba 24, 2025, Katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, Donald Mwembe amesema kitendo cha Jeshi la Polisi kumshikilia Heche bila kueleza alipo kimezua taharuki ndani ya jamii.
“Heche si kiongozi wa familia yake tu, mbali na kuwa mwanachama wangu, lakini ni kiongozi anayewakilisha jumuiya kubwa ya Watanzania nchini kote, hususan wale wapenda haki na dekomkrasia,” amesema.
Amesema kuwa ukimya wa polisi juu ya alipo kiongozi huyo unasababisha hofu kubwa miongoni mwa Watanzania, hasa ikizingatiwa vitendo vya watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha vimekuwa vikitokea mara kwa mara.
Mwembe amesisitiza kuwa ni vema Jeshi la Polisi likaweka wazi tuhuma lilizonazo dhidi ya kiongozi huyo, ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Aidha, amebainisha kuwa kitendo cha polisi kumkamata mtu na kukaa kimya bila kueleza alipo au tuhuma zake si tu kimevunja haki za binadamu, bali pia ni kinyume cha kanuni za utawala bora.
Mwembe amesema viongozi wa dini, watu mashuhuri, wanaharakati wa haki za binadamu na makundi mbalimbali katika jamii, kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kujitokeza na kupaza sauti juu ya hali hiyo aliyosema kuwa ni uonevu.
“Hakuna aliye salama, hivyo kila mtu kwa nafasi yake apaze sauti kukemea vitendo vya aina hii, lakini pia kwa pamoja tulitake Jeshi la Polisi kutuambia alipo Heche,” amesema.
Jana Oktoba 23, 2025 familia ya Heche ilitoa muda hadi leo saa 3 asubuhi kwa Jeshi la Polisi kujitokeza na kusema alipo ndugu yao, la sivyo wangeshirikana na wananchi kumasaka popote pale alipo.
Mdogo wa Heche, Chacha Heche alisema wameamua kutoa muda huo ili kuonyesha namna gani walivyowavumilivu na kwamba hawataki kuzua taharuki yoyote.
Alisema familia haiko tayari kuona ndugu yao akipoteza maisha bila sababu ya msingi, kwani wanaamini hana makosa ya aina yoyote zaidi amekuwa mstari wa mbele kudai haki na demokrasia kwa ustawi wa nchi na watu wake.
Chacha alisema baada ya ndugu yao kukamatwa walipewa taarifa kuwa angesafirishwa kwenda Tarime, lakini hadi jana alikuwa hajafika wala hawakuwa na taarifa juu yake huku zikiwepo danadana kuhusu alipo.
Akizungumza suala hilo leo, Chacha amesema wamesitisha kwa muda shughuli ya kumtafuta ndugu yao iliyotarajiwa kuanza leo baada ya kuzuiliwa kwa muda na chama chao.
“Chama makao makuu wametuzuia kwa muda, tunasubiri tamko lao kisha tuendelee na utaratibu wetu, ninachoweza kusema ni kwamba hadi sasa hatuna taarifa juu ya alipo ndugu yetu,” amesema Chacha.
