Dar es Salaam. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Devotha Minja amewataka Watanzania kufanya uamuzi sahihi Oktoba 29, kwa mustakabali maisha yao.
Amesema nyakati za ahadi zisizotekelezeka umepitwa na wakati badala yake Watanzania wanahitaji chama kitakachotekeleza kile kinachoahidiwa na si kingine ni Chaumma.
Minja ambaye kitaaluma ni mwanahabari ameeleza hayo leo Ijumaa Oktoba 24, 2025 wakati akimnadi mgombea ubunge wa Kinondoni, Moza Ally katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Ali Maua Kijitonyama.
“Nimekuja kuwambusha ndugu zangu tukafanye uamuzi mgumu wa kuiondoa CCM ifikapo Oktoba 29. Nimezunguka sana nchi hii, kina mama wana maisha magumu, hawana furaha, wamechoka, halafu wanasema tukatiki, tukatiki nini?
“Niwaombe wananchi wa Kinondoni, hakikisheni mnakipa Chaumma kura kuanzia Rais, mbunge (Moza) na madiwani. Chaumma tutaleta heshima kwa Watanzania, tutafumua mfumo wa ajira na tutarejesha viwanda vilivyokufa, huduma za uhakika hospitalini,” amesema Minja.
Minja amesema kwa nyakati tofauti, CCM iliahidi matibabu bure, maisha bora kwa kila Mtanzania, lakini sasa bado wananchi hawajayaona hayo maisha bora zaidi ya ugumu wa maisha.
“Waliahidi wataondoa ada ana michango shuleni, leo michango ipo au haipo? Akajibiwa bado ipo na wananchi. Walituambia kuwa watahakikisha watahakikisha wataongeza kipato kwa mwananchi, naomba kujua kipato kimeongezeka? Akajibiwa bado.
Minja amesema Watanzania wakiwemo kina mama wamesomesha watoto wao kwa tabu ikiwemo kufanya biashara za mbogamboga ili kuhakikisha wanapata elimu bora.
“Kina mama wamefunga mkanda wamesomesha watoto wao hadi chuo kikuu, lakini watoto wapo nyumbani hawana ajira. CCM imeshindwa kutengeneza ajira kwa vijana wetu, kuna walimu wamesomea vizuri lakini hawana ajira wapo nyumbani,” amedai Minja.
Kwa upande wake, Moza amewaahidi wananchi wa Kinondoni ndani ya siku 100 atahakikisha kero ya maji inapata ufumbuzi ili kuleta ahueni ya huduma hiyo katika jimbo hilo.
“Wananchi wenzangu, kina mama wenzangu naijua hii shida ya maji nitakwenda kuisimamia. Nitakwenda kuipigania, nasikia hata yakitoka yanakuwa ya chumvi, nipe kura nitakwenda kuwa sauti yenu wananchi wa Kinondoni,” amesema Moza.
Mbali na hilo, Moza amesema katika kuhakikisha wananchi wa jimbo wapata mikopo kwa ufanisi atahakikisha anaweka utaratibu bora ili kila mwenye sifa ananufaika na mchakato huo.
“Nitakuwa na timu ya watu wawili pale ofisi ya mbunge, itakayowasaidia namna ya kuandika Katiba zenu na msaada wa kisheria pindi mtakapokwama. Mniamini nipeni kura mtaondokana na mikopo ya kausha damu nimedhamilia kutatua changamoto hii,”amesema Moza.
Wakati huo huo, mgomb ea mwenza huyo, Devotha Minja, amewataka wanawake wa jimbo la Mbagala na Watanzania kwa ujumla wachague wagombea wa Chaumma kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani ili kuleta mabadiliko ya kweli nchini.
Akizungumza leo Ijumaa, Oktoba 24, 2025, katika mkutano wa kampeni wa chama hicho uliofanyika Kata ya Kiburugwa, Jimbo la Mbagala, Dar es Salaam, Minja amesema ni wakati wa wanawake kuamka na kuchagua viongozi watakaopigania maisha yao, si wanaowapa ahadi zisizotekelezeka kila uchaguzi.
“Kinamama, muda wa kuachana na ahadi hewa umefika. Tumechoshwa na Serikali ya CCM ambayo imewaacha kwenye umasikini, imewashusha heshima na kuwabebesha mikopo yenye masharti magumu, mabadiliko ni Chaumma,” amesema Minja.
Amesema Serikali ya sasa imeshindwa kuwakomboa Watanzania, hasa wanawake, ambao wamekuwa wakihangaika na biashara ndogondogo zisizo na tija huku wakikosa mitaji ya uhakika.
“Tukipewa ridhaa, tutahakikisha wanawake wanapata mikopo isiyo na masharti magumu na yenye riba ndogo. Hatutaki tena kuona mama analipa mkopo kwa kuuza vyombo na mali zake za ndani, tunataka maendeleo yenye utu,” amesema.
Katika mkutano huo. mgombea ubunge wa Mbagala kwa tiketi ya Chaumma, Hadija Mwago, amewahutubia wananchi na kuwataka wamchague ili aende Bungeni kuboresha maisha yao na kuwakomboa kiuchumi.
Mwago amesema wakazi wa jimbo hilo wameendelea kuishi maisha duni, hali inayowalazimisha kula vyakula vya bei nafuu kama miguu na utumbo wa kuku, huku viongozi wa chama tawala wakiishi maisha ya anasa katika maeneo ya kifahari kama Masaki.
“Hivi ndugu zangu hawa wanaosema wanatuletea maendeleo, wao huko Masaki wanakula utumbo na miguu kweli? Wanasema wametujengea shule na hospitali za maghorofa, lakini nyinyi wanambagala mnayaona hayo maghorofa?” amehoji Mwago.
Amesema endapo atachaguliwa kuwa mbunge, ataweka kipaumbele katika kuanzisha kituo cha mafunzo ya ajira kwa vijana kitakachowapa ujuzi na maarifa ya kiufundi ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.
“Mkinichagua, hapa Mbagala nitaanzisha kituo cha mafunzo ya ajira kwa vijana yatakayowawezesha kupata maarifa na ajira. Vijana wetu hawana fursa, tutawapatia mwelekeo wa kiuchumi,” amesema Mwago.
