Mbeya. Mgombea ubunge wa Jimbo la Uyole, Dk Tulia Ackson, ameanza kampeni za nyumba kwa nyumba na mtaa kwa mtaa kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, kwa nafasi ya Rais, wabunge na madiwani.
Mbali na hatua hiyo, amekuwa akitembea akiwa na bango lenye picha yake pamoja na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, jambo ambalo limekuwa kivutio kwa wananchi.
Katika kampeni zake za mguu kwa mguu Dk Tulia leo Oktoba 24,3025 amezifikia kata za Mwasekwa na Ilemi kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi Oktoba29, 2025.
“Jitokezeni kupiga kura katika uchaguzi mkuu ili kutimiza haki yenu kisheria kuchagua Rais, wabunge na madiwani waweze kuleta maendeleo kipindi cha miaka mitano ijayo,”amesema.
Katika hatua nyingine, Dk Tulia amewataka wananchi kupiga kura kwa amani na kutojihusisha na maandamano au vurugu yoyote, akisisitiza badala yake kulinda amani iliyowekwa na mwasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere.
“Siku ya Jumatano Oktoba 29, 2025, siku muhimu kwa Watanzania mkapige kura kumchagua Rais Samia Suluhu Hassan na mimi mbunge wenu Dk Tulia, lakini pia madiwani wa kata zote 13 za jimbo la Uyole,” amesema.
