HESLB YATENGA SH426.5 BILIONI KWA MIKOPO NA RUZUKU KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU


:::::::::

Na Mwandishi Wetu, 

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kutoa mikopo na ruzuku zenye jumla ya Sh426.5 bilioni kwa wanafunzi 135,240 wa elimu ya juu nchini kwa mwaka wa masomo 2025/2026, ikiwa ni awamu ya kwanza ya upangaji wa mikopo na ufadhili wa *Samia Scholarship*.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa, Oktoba 24, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk Bill Kiwia, alisema fedha hizo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali ya awamu ya sita wa kuhakikisha kila mwanafunzi mwenye sifa na uhitaji anapata msaada wa kifedha ili kuendelea na masomo bila vikwazo vya kiuchumi.

“Kati ya wanafunzi hao 135,240, wanafunzi 40,952 wa shahada ya awali na 5,342 wa stashahada wamepangiwa mikopo yenye jumla ya Sh152 bilioni,” alisema Dk Kiwia.

Aidha, alisema wanafunzi 615 waliopata ufadhili wa *Samia Scholarship* wamepangiwa ruzuku yenye thamani ya Sh3.3 bilioni, huku wanafunzi 88,331 wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali nchini wakipangiwa mikopo yenye jumla ya Sh271.2 bilioni.

Dk Kiwia alifafanua kuwa wanafunzi waliopangiwa mikopo na ruzuku katika awamu hii ni wale waliowasilisha maombi yao kuanzia Juni 15 hadi Septemba 15, 2025.

Ameongeza kuwa HESLB itaendelea kutoa awamu nyingine za mikopo na ruzuku kadiri inavyopokea uthibitisho wa udahili wa wanafunzi wapya na matokeo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo.

Kwa mujibu wa Dk Kiwia, Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa utoaji mikopo na ufadhili wa elimu ya juu kwa lengo la kuongeza fursa za elimu kwa Watanzania wote wenye uwezo wa kitaaluma lakini wasio na uwezo wa kifedha.