HESLB yatoa Sh426.5 bilioni kwa wanafunzi 135,240 wa elimu ya juu

Arusha. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa mikopo na ruzuku yenye thamani ya Sh426.5 bilioni kwa wanafunzi 135,240 wa elimu ya juu nchini kwa mwaka wa masomo 2025/2026 ikiwa ni awamu ya kwanza ya upangaji wa mikopo na ufadhili wa Samia Scholarship.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Oktoba 24, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk Bill Kiwia amesema fedha hizo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuhakikisha kila mwanafunzi mwenye sifa na uhitaji anapata msaada wa kifedha ili kuendelea na masomo bila vikwazo vya kiuchumi.

Amesema wanafunzi hawa ni wale waliowasilisha maombi yao kuanzia Juni 15 hadi Septemba 15, 2025.

“Kati ya wanafunzi hao 135,240, wanafunzi 40,952 wa shahada ya awali na 5,342 wa stashahada wamepangiwa mikopo yenye jumla ya Sh152 bilioni,” amesema Dk Kiwia.

Aidha, wanafunzi 615 waliofanikiwa kupata Samia Scholarship wamepangiwa ruzuku yenye thamani ya Sh3.3 bilioni huku wanafunzi 88,331 wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali nchini wakipangiwa mikopo yenye jumla ya Sh271.2 bilioni.

Dk Kiwia amesema HESLB itaendelea kutoa awamu nyingine za mikopo na ruzuku kadiri inavyopokea uthibitisho wa udahili wa wanafunzi wapya na matokeo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo.

“Tunawahimiza waombaji wote kufuatilia taarifa za maombi yao kupitia akaunti zao za SIPA. Hii ndiyo njia rasmi ya kupata taarifa sahihi wakati taratibu za uchambuzi na upangaji wa mikopo zinaendelea,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa Dk Kiwia, Serikali imetenga Sh916.7 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kugharamia mikopo ya wanafunzi 273,347, wakiwemo 99,300 wa mwaka wa kwanza na 174,047 wanaoendelea na masomo.

Amesema kiasi hicho ni ongezeko kutoka Sh787 bilioni zilizotolewa mwaka uliopita kwa wanafunzi zaidi ya 245,000.

“Ongezeko hili linaonyesha dhamira ya Serikali kuwekeza zaidi katika elimu ya juu kama nguzo ya maendeleo ya taifa. Tunataka kuona vijana wengi zaidi wakipata nafasi ya kufikia ndoto zao bila kikwazo cha kifedha,” amesema.

Amesema kuwa HESLB imejipanga kuhakikisha fedha za mikopo zinawafikia walengwa mara baada ya kuwasili shuleni Novemba 3, 2025 ili wanafunzi waanze masomo kwa wakati bila usumbufu.

Aidha, amewapongeza wanufaika wa mikopo wanaoendelea kurejesha madeni yao kwa hiari, akisema hatua hiyo inaongeza uwezo wa bodi kugharamia kizazi kingine cha wanafunzi.

Amesema kwa sasa mikopo ambayo imeiva inakaribia Sh2.7 trilioni na kati yake wanakusanya Sh1.8 trilioni ambayo ni zaidi ya asilimia 70.

“Katika ukusanyaji huo kwa mwezi tunakusanya zaidi ya Sh20 bilioni, kitendo kinachoifanya Tanzania kuongoza Afrika kwa ukusanyaji wa madeni ya mikopo hiyo,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo kutoka HESLB, Dk Peter Mmari ametumia nafasi hiyo kuwataka waombaji wote na umma kwa ujumla kupata taarifa sahihi kupitia tovuti rasmi ya bodi na kurasa zake za mitandao ya kijamii kwa jina la HESLB Tanzania, kuepuka upotoshaji kutoka vyanzo visivyo rasmi.

Amesema taasisi hiyo itaendelea kuimarisha mifumo ya kidigitali ili kuongeza uwazi, ufanisi na wepesi katika utoaji wa mikopo na urejeshaji wake.

“Tunaendelea kuwa taasisi ya mfano barani Afrika katika kusaidia vijana kupata elimu ya juu kupitia mifumo bora, yenye uwazi na inayozingatia usawa, kikubwa hakuna mwenye sifa ataekosa mkopo bali wawe wanatimiza masharti yaliyowekwa na kufuatilia mitandao sahihi,” amesema.