Job awaita mashabiki kwa Mkapa kesho

BAADA ya Yanga kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Silver Strikers Oktoba 18, 2025, beki na nahodha msaidizi wa timu hiyo, Dickson Job amesema hawatakubali unyonge kufungwa tena nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa, kesho Jumamosi Oktoba 25, 2025.

Job amesema mechi hiyo ni ya kurejesha heshima kwa Klabu ya Yanga, kuhakikisha wanapambana ili kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF).

Yanga kesho Jumamosi itakuwa mwenyeji wa Silver Strikers katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania kufuzu makundi.

Kufuatia kufungwa 1-0 ugenini mechi iliyopita, Yanga inatakiwa kushinda angalau kwa tofauti ya mabao 2-0 ili kufuzu makundi, lakini ikishinda 1-0, mikwaju ya penalti itaamua. Ikiwa tofauti na hapo, safari yao itakuwa imefika mwisho.

“Nipo hapa kuwawakilisha wachezaji wenzangu kuwaambia tunajua mechi hiyo ni muhimu sana kushinda, tutapambana kwa jasho na damu ili tutinge hatua ya makundi,” amesema Job na kuongeza;

JOB Pict

“Nawaomba mashabiki kesho wajue tuna jambo muhimu uwanja wa Mkapa, wajitokeze kwa wingi kutusapoti, umoja wetu utatupa matunda na furaha.”

Job amesema kufungwa ugenini hakuna maana kwamba Yanga imefeli, bali plani ambazo walienda nazo hazikufanya kazi, hivyo awamu hii watakwenda kivingine.

“Mashabiki wetu waendelee kuweka imani na sisi, kesho wataondoka kifua mbele, hatutawaangusha, lazima brandi ya timu itaheshimika,” amesema Job.

Katika kuweka uzito wa mechi hiyo, Yanga imetangaza haitakuwa na kiingilio, hivyo mashabiki wataingia bure.