KONA YA MSTAAFU: Iko wapi nchi ya asali na maziwa kwa wastaafu?

Miaka 48 iliyopita wakati tukianza ajira moja kwa moja kutoka shule, mashirika, kampuni za umma na binafsi zilituajiri bila kulazimika kuwa na tochi kutafuta ajira, kama ilivyo sasa, tulikuwa tunaelekea kwenye nchi ya asali na maziwa.

Kibubu pekee kilichokuwepo enzi hizo cha akiba ya wafanyakazi cha NPF, kikaanza kutuwekea akiba iliyoikata kutoka kwenye mishahara yetu kilituaminisha, tukaamini, kuwa nchi ya asali na maziwa ilikuwa inatuhusu pale tutakapostaafu miaka 40 baadaye, sasa!

 Baada ya ‘kuustaafu’ kwetu tukiwa wazee wa miaka 60,  tumekua tukishuhudia  waajiriwa wachache waliokuwa wenzetu  tulioanza nao kazi, ambao ghafla sasa hawajui hata maana ya neno ‘kustaafu,’ acha kustaafu’ kwenyewe, huku baadhi ya hao wachache wakiwa na miaka hata 80 lakini bado wanateuliwa kuwa wenyekiti wa tume hii, ama wenyemeza wa tume Ile !

Mstaafu wetu huyu anaposikia teuzi hizi za waajiriwa wenzetu hufikia kujiuliza kama wanalipwa mishahara au pensheni kutokana teuzi na uzee wao, huku vijana wetu waliomaliza vyuo vyetu vikuu tulivyonavyo rundo wakiishia kusaka ajira kwa tochi, huku ajira zinazoonekana, ziikishia kuhodhiwa na ‘wastaafu’ wanaopaswa kustaafu’ kuwapisha vijana wetu.

Achieni ngazi vijana wetu wapate kazi.

Uzoefu unaotakiwa ili kupata ajira hizo, bila kuzisaka kwanza kwa tochi, wataupata wapi?

Wale walioajiriwa miaka ya 60 na 70, akina sisi, waliupata wapi uzoefu huo na wakaweza kuijenga na kuilinda nchi? Wastaafu wenzetu wawape vijana kazi watufundishe mambo mapya, uzoefu wataupata humo humo !

Haya, baada ya miaka 40 ya ajira tukiwa na miaka 60, sheria tuliyojiwekea wenyewe ikatutaka tuachie ngazi tuwe wastaafu, ili mchuma uondoke!

Wenzetu wakiendelea na ajira pamoja na miaka 60 yao, sisi wengine tuliopigwa kibuti na kuachia ngazi tukabaki kuwa bize kuzungusha shingo na macho yetu ya kizee kuiona hiyo nchi ya ‘asali na maziwa’ tuliyoaminishwa kwamba itakuwepo tukiistafu!

Tumeumia bure kuzungusha shingo tukitafuta ‘ nchi ya asali na maziwa’ kwa wastaafu, wakati nchi sasa imekuwa ya kikokotoo kwa wataafu ambao walipoanza kukatwa mishhara yao na NPF ili miaka 40 baadaye nchi iwe ya ‘asali na maziwa’ kwa wastaafu, neno ‘ kikokotoo’ lilikuwa hata halijavumbuliwa!

Badala ya nchi ya ‘asali na maziwa’ kwa wastaafu, kibubu cha akiba yake sasa kimekuwa nchi ya mikopo na anayetaka kujikopesha bila tozo na riba husika   anapiga hodi kwenye kibubu cha akiba ya wastaafu kukopeshwa hela ya wastaafu’, kujenga vikwangua anga vya kuuza ama kukodisha huku kibubu hicho hakina mkopo wa kumsaidia mwenye hela zake, mstaafu!

Na sasa kumefikia hali ya hatari ya watu kuchukua hela ya kibubu cha mstaafu kwenda kufanya matumizi na matanuzi na kumfanya mstaafu asipokee pensheni yake ya mwezi ya shilingi laki moja na alfu hamsini kwa miezi miwili ije kumlipa mwezi wa tatu shilingi laki nne na alfu hamsini zilizopaswa kuwa nyongeza ya pensheni ya mstaafu!

Waheshimiwa, acheni michezo na maisha ya wastaafu’ waliostaafu kwa Amani. Laki si pesa yao mnaikopa ya nini? Matumizi na matanuzi yenu hayawatoshi mpaka mjikopeshe hela ya mstaafu na kumfanya akae miezi miwili mizima bila chochote.

Nchi ya asali na maziwa kwa mstaafu imeishia sasa kuwa ya maumivu ya kuumwa na nyuki.

Kuna mheshimiwa alituambia kwamba hatuelewani na kinachoendelea nchini basi tuchape lapa na twende Burundi, sijui huko tutampigia nani tunayemfamu kura zetu!

 0754 340606 /. 0784 340606