Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imelikataa ombi la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu la kutaka apewe dhamana. Lissu aliwasilisha hoja hiyo leo Ijumaa, Oktoba 24, 2025 baada ya Jamhuri kuomba kesi iahirishwe kutokana na kutokuwa na shahidi kwa siku ya leo.
Awali, Jamhuri katika kesi hiyo ya uhaini inayomkabili Lissu, iliomba iahirishwe mpaka Novemba 3, 2025 kwa kuwa leo hawana shahidi.
Kesi hiyo inayosikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde ilitarajiwa kuendelea kusikilizwa leo Oktoba 24, 2025.
Hata hivyo, Jamhuri imeieleza Mahakama kuwa kwa leo hawana shahidi kwa kuwa mashahidi waliokuwa wanafuata kutoa ushahidi wao unahusiana na vielelezo vilivyokataliwa Oktoba 22 na 23, 2025.
Vielelezo hivyo ni vihifadhi data (flash disk na memory card) zenye picha mjongeo yenye hotuba ya Lissu yenye maudhui yanayodaiwa kuwa na maneno ya kuitishia Serikali ambalo ni kosa la uhaini.
Wakili wa Serikali Mkuu, Lenatus Mkude amesema kuwa kwa kuwa leo ni siku ya mwisho ya kikao cha usikilizwaji wa kesi hiyo basi wanaomba kesi hiyo iahirishwe chini ya kifungu cha 302 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) mpaka Novemba 3, 2025 kama ratiba ya usikilizaji kesi hiyo inayoonesha.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendelealo (Chadema), Tundu Lissu akiwa chini ya ulinzi wakati akiwasili katika Mahakama Kuu leo Ijumaa Oktoba 24, 2025. Picha na Ally Mlanzi.
Hata hivyo, Lissu amepinga ombi hilo akisema sababu iliyotolewa na upande wa Jamhuri haina msingi na akaiomba mahakama kuumuru upande wa mashtaka ulete shahidi ili kesi iendelee.
Amedai kuwa baada ya vielelezo hivyo kukataliwa hakuna kesi tena na kwamba, hakuna ushahidi mwingine wa kuthibitisha shitaka hilo.
Akaiomba mahakama hiyo kwamba kama inakubaliana na ombi hilo la Jamhuri na kuataka kesi iahirishwe basi impatie dhamana kwa mujibu wa kifungu cha 302(2) cha CPA.
Jopo la mawakili wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendelealo (Chadema), Tundu Lissu wakiwa katika Mahakama Kuu leo Ijumaa Oktoba 24, 2025. Picha na Ally Mlanzi.
Lakini, Wakili Mkude na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga wamepinga hoja ya maombi hayo ya Lissu kutaka kupewa dhamana wakidai shitaka linalomkabili kisheria halina dhamana.
Akitoa uamuzi wa mahamama, Jaji Ndunguru amekubaliana na maombi na hoja za Jamhuri akisema kuwa sababu ya ombi la ahirisho ni la msingi na ya kisheria.
Pia amesema ingawa kifungu alichokitaja Lissu kuomba dhamana kinatoa mazingira, lakini sababu ya ahirisho iliyotolewa ni ya kisheria na kwamba pia shitaka linalomkabili halina dhamana.
“Kwa kuwa leo ndio mwisho wa session (kikao) hii, shauri hili linaahirishwa mpaka Novemba 3, 2025, kama cause list (ratiba ya mahakama ya usikilizwaji kesi hiyo) inavyoonesha,” alimaliza Jaji Ndunguru.
Kwa uamuzi huo, Lissu amerudishwa rumande huku akitimiza siku ya 202 rumande tangu alipokamatwa Aprili 9, 2025 na kufunguliwa kesi hiyo.
