Mashujaa yapiga mkwara ikiikaribisha Namungo

MASHUJAA imeahidi kufanya vizuri dhidi ya Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, kesho.

Mashujaa imepata matokeo yasiyoridhisha katika mechi zake mbili mfululizo zilizopita ambapo katika mechi moja ilifungwa mabao 2 -1 na Pamba ya Mwanza na kisha kuambulia sare ya bila kufungana na TRA United ya Tabora.

Akizungumza leo na waandishi wa habari, kocha mkuu wa Mashujaa, Salum Mayanga amesema wamerekebisha makosa waliyoyafanya kwenye michezo iliyopita.

“Vijana wapo vizuri kukabiliana na timu ya Namungo siku ya kesho na matumaini yangu tutacheza kwa kujituma, juhudi na matumaini yangu tutapata ushindi,” amesema Mayanga.

Mchezaji wa Mashujaa, Frank Magingi amesema wamejipanga na watautumia vizuri uwanja wa nyumbani kuondoka na ushidi dhidi ya Namungo, hivyo washabiki wajitokeze kwa wingi kupata burudani.

Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda amesema wapo tayari kucheza na Mashujaa ambayo ni timu bora na yenye kocha mwenye uzoefu, lakini wanajua vizuri timu wanayokwenda kupambana nayo.

“Hadi sasa vijana wapo vizuri na nawaombea kwa Mungu waamke salama kwani haki na wajibu hivyo waende wakatimize wajibu wao na naamini tutafanya vizuri kwani tumejipanga ikiwemo maandalizi ya kutosha,” amesema Mgunda.

Mchezaji wa Namungo, Abdallah Mfuko amesema kila mchezo kwao una umuhimu na wanakwenda kupambana ili wapate matokeo mazuri.