Mavituz ya Pantev Simba yamkosha Mbrazili

MASHABIKI wa Simba tabasamu limeanza kurudi kwenye nyuso zao kutokana na mwenendo wa kikosi hicho katika mashindano mbalimbali.

Wakati hayo yakiendelea kocha wao wa zamani amewatumia salamu akisema meneja mpya, Dimitar Pantev ana kitu cha maana anachokiwekeza kikosini hivyo waishi naye vizuri.

Unaweza kusema Pantev ameshusha presha Simba baada ya kuiongoza kushinda kibabe ugenini kwa mabao 0-3 dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini, na sasa imerudi nyumbani kumalizia kazi ili kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambaye kwa sasa yupo Saudi Arabia akiifundisha Jeddah SC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, amesema alifuatilia mechi ya Nsingizini dhidi ya Simba na kubaini Wekundu wa Msimbazi wamebadilika kiuchezaji.

Kilichomvutia Robertinho ni Simba inacheza soka la kasi kuelekea lango la wapinzani, kitu ambacho ni muhimu kwa soka la kisasa, huku akisema Pantev akiendelea na falsafa hiyo basi kikosi hicho kitatisha zaidi.

PANT 01

Robertinho aliyetua Simba Januari 3, 2023 na kuondoka Novemba 9, 2023 akishinda Ngao ya Jamii, amesema falsafa za Pantev, hazitofautiani sana na kile alichokuwa anajaribu kukijenga wakati akiifundisha timu hiyo na kikosi hicho lazima kiwe hatari kwa kuwa na kasi wakati wapinzani wanapopoteza mpira.

“Nilipambana sana kuangalia ile mechi iliyocheza Simba na timu ya Eswatini (Nsingizini), nilivutiwa na namna timu ilivyocheza, huyu kocha mpya (Pantev) akili yake ni kama yangu, inawezekana tukawa tunatofautiana kidogo sana,” amesema Robertinho.

“Simba inacheza soka la malengo, unaona ilivyo na kasi wakati inaukamata mpira, wanakimbia sana kuwahi lango la wapinzani, hii ni nzuri sana kama itaendelezwa na huyu kocha akipewa muda abadilishe mambo.”

PANT 02

Robertinho alivutiwa na baadhi ya mastaa wapya wa Simba akisema kikosi hicho kilikuwa imara kwenye safu zake tatu kuanzia ulinzi, katikati na safu ya ushambuliaji akimwagia sifa Kibu Denis.

“Wanacheza vizuri eneo la ulinzi, ile timu (Nsingizini) siyo rahisi, ni nzuri, ilikuwa inatengeneza kitu lakini ukuta wa Simba ulikuwa imara zaidi kuzima hayo yote.

“Angalia pia katikati wana viungo wazuri, kuna viungo wengine waliingia kipindi cha pili, walibadilisha mchezo sana, walikuwa na akili kubwa ya kuwaadhibu wapinzani wakati wanataka kutafuta bao la kusawazisha.

PANT 03

“Washambuliaji nao walikuwa wanamaliza kazi vizuri, nimefurahi kumwona Kibu akifunga mabao mawili, unakumbuka nilikwambia Kibu ni mchezaji mzuri sana,” amesema Robertinho.

Robertinho amesema anawataka viongozi wa Simba kumpa muda Pantev abadili mambo ndani ya timu hiyo bila kumwingilia ili kikosi hicho kirudi kwenye ubora zaidi.

Simba itarudi uwanjani Oktoba 26, 2025 kumalizana na Nsingizini kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar ikihitaji sare au ushindi wowote na kama ikifungwa basi isiwe kwa zaidi ya mabao 2-0 ili kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ugenini kushinda 0-3.

Mshambuliaji wa Simba, Jonathan Sowah aliliambia Mwanaspoti kuna kitu ambacho amemshtukia kocha Pantev, hasa anapompatia mchezaji nafasi.

Sowah ambaye kwenye mechi dhidi ya Nsingizini aliingia mwanzoni mwa kipindi cha pili akichukua nafasi ya Seleman Mwalimu, amesema: “Kocha Pantev anataka akikupa nafasi ufanye kitu cha tofauti na hicho ndicho kila mchezaji anakipigania, haijalishi ni muda kiasi gani anakupa.

PANT 04

“Kama sio kufunga basi anataka ushiriki kutoa hata asisti ili timu ipate kitu tofauti, unajua tuna timu nzuri ambayo kuendelea kushinda itaongeza morali na kuongeza kiu ya kufikia malengo yetu.”

Aliongeza kuwa: “Ushindani wa namba uliopo kwa sasa ni mkali kwani kila mmoja anataka kuonyesha kiwango chake kwa kocha kwamba anastahili kucheza hasa hizi mechi za kimataifa.”