Mbeya City, JKT Tanzania ni vita ya kileleni Ligi Kuu

LIGI Kuu Bara inaendelea leo Ijumaa kwa mechi moja kupigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam na Mbeya City iliyochapwa na Tanzania Prisons mabao 2-1, itajiuliza dhidi ya JKT Tanzania iliyotoka sare ya bao 1-1 na Namungo.

Mbeya City iliyorejea Ligi Kuu msimu huu baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, imecheza mechi tano hadi sasa na kati ya hizo imeshinda mbili, ikianza na bao 1-0, dhidi ya Fountain Gate Septemba 18, 2025 kisha 3-0 na KMC Oktoba 18, 2025.

Mechi mbili imechapwa, ikianza kwa kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Azam FC, Septemba 24, 2025 kisha kuchapwa na maafande wa Tanzania Prisons katika ‘Mbeya Derby’, Oktoba 21, 2025 huku ikitoka suluhu (0-0), mbele ya Yanga jijini Mbeya, Septemba 30, 2025.

Kwa upande wa JKT Tanzania, katika mechi nne ilizocheza msimu huu, imeshinda moja tu ambayo ni ya ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya Coastal Union, Septemba 22, 2025, huku mitatu ikitoka sare ikianza na ya bao 1-1, mbele ya Mashujaa FC, Septemba 18, 2025.

MBEY 01

Sare nyingine ya kikosi hicho cha maafande ni ya bao 1-1 dhidi ya matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC, Oktoba 1, 2025, kama ilivyokuwa pia mechi ya mwisho iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo iliyoisha 1-1 na Namungo Oktoba 19, 2025.

Katika mechi tano ilizocheza Mbeya City, imeshinda mbili, ikitoka sare moja na kupoteza mbili, ikiongoza kileleni na pointi saba, huku kwa upande wa JKT Tanzania, ikishinda moja na kutoka sare tatu, ikiwa nafasi ya nne na pointi sita.

Ushindi kwa Mbeya City utaifanya kuendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu huu, ingawa endapo kikosi hicho cha maafande wa JKT Tanzania kitaibuka kidedea, kitaruka hadi nafasi ya kwanza kwa kufikisha jumla ya pointi tisa.

Timu hizi zinakutana kwa mara ya kwanza tangu mara ya mwisho zilipokutana katika Ligi Kuu Bara, Aprili 28, 2021 na kikosi hicho cha Mbeya City kinakumbukumbu nzuri, kwa sababu kwenye pambano hilo kiliibuka na ushindi mnono wa mabao 6-1.

Mabao ya Mbeya City yalifungwa na Kibu Denis anayeichezea Simba kwa sasa kunako dakika ya 18, David Mwasa dakika ya 45, Richardson Ng’ondya dakika ya 50 na Pastory Athanas dakika ya 90, huku Juma Liuzio akifunga mawili dakika ya 68 na 88.

MBEY 02

Bao pekee la kufutia machozi la JKT Tanzania katika mechi hiyo, lilifungwa na Daniel Lyanga dakika ya saba, huku mara ya mwisho kwa maafande hao kuifunga Mbeya City katika Ligi Kuu Bara ilikuwa ushindi wa 1-0, Novemba 6, 2019.

Kocha wa Mbeya City, Malale Hamsini, amesema wamefanyia kazi eneo lote la ushambuliaji kutokana na kukosa nafasi nyingi za kufunga katika pambano la mwisho, huku Ahmad Ally wa JKT Tanzania, akiwataka wachezaji kucheza kwa tahadhari kubwa.