Mechi mbili zijazo ni moto kwa Maximo

MZEE wetu Marcio Maximo aliingia kwa matumaini makubwa ndani ya timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) kama kocha mkuu kwa ajili ya msimu huu.

Kwa kumbukumbu za hapa kijiweni, huu ni ujio wa tatu kwa Maximo nchini kwani mara ya kwanza alikuja kuinoa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kisha mara ya pili alikuja kuifundisha Yanga.

Alipokuja kuikochi Taifa Stars, Maximo ndio alijitengenezea heshima nchini kwani aliweza kuiunganisha nchi na kuifanya iwe kitu kimoja na iisapoti timu ya taifa na alifanikiwa kwelikweli katika hilo.

Mara ya pili alipokuja ambapo aliletwa na Yanga, mambo hayakumuendea vizuri na hakudumu sana kwani baada ya muda mfupi pande hizo mbili zilifikia makubaliano ya kuachana.

Sasa hii mara ya tatu alipokuja hapa kijiweni tukawa tunaamini kwamba atatumia fursa hiyo kuthibitisha kuwa kilichotokea Yanga kilikuwa ni ajali tu ambayo imechangiwa na presha kubwa ya matokeo mazuri ambayo timu hiyo imekuwa nayo kwa miaka mingi.

Tukaamini kwamba KMC chini yake itakuwa moto wa kuotea mbali kwa vile kwanza haina presha kubwa na pia haina malengo makubwa hivyo Maximo ataifanya kazi yake kwa utulivu wa hali ya juu na mwisho atafanikiwa kutengeneza timu tishio.

Lakini mambo hayaonekani kumuendea vizuri mzee wetu Marcio Maximo kwani hadi sasa timu yake imepata ushindi katika mechi moja tu kati ya tatu ambazo imecheza huku ikipoteza michezo miwili ambayo yote ilikuwa nyumbani na mmojawapo ilichapwa mabao 3-0 na Mbeya City.

Jambo gumu zaidi kwa KMC ni kwamba ina mechi mbili zinazofuata ambazo zote itakuwa ugenini dhidi ya Foutain Gate na Yanga ambazo ikipoteza maana yake itaporomoka zaidi.

Kijiwe hakioni kama Marcio Maximo anaweza kuwa salama kama KMC itapoteza mechi hizo mbili zinazofuata. Ni ngumu kuwa na uvumilivu huo.