Mwanza. Mgombea urais wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Wilson Elias, amesema endapo chama chake kitapata ridhaa ya kuongoza nchi, kitasimika satelaiti angani kwa ajili ya kudhibiti uhalifu unaofanyika katika maziwa ya Victoria na Tanganyika, pamoja na kulinda mipaka ya nchi kwa ujumla.
Ahadi hiyo ameitoa Oktoba 23, 2025 alipofanya mikutano ya hadhara Kayenze na Kisiwa cha Bezi mkoani Mwanza, ikiwa ni mwendelezo wake wa kuomba kura mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Elias amesema satelaiti hiyo itakayosimikwa katika eneo lisiloonekana kwa macho ya kawaida itasaidia kulinda wavuvi dhidi ya matukio ya uporaji na uvamizi ambayo yamekuwa yakiwakumba wakiwa majini.
“Kilio cha wavuvi kinafanana kila mahali. Kumekuwa na majangili na majambazi ndani ya maziwa. Serikali yangu itaweka satelaiti angani eneo ambalo hakuna mtu anaweza kuona.
“Hii itaimarisha ulinzi kwenye maziwa pamoja na mipaka yetu yote, kwa hiyo maadui mwisho wao utakuwa umefika mtakapotuchagua ADC,” amesema Elias.
Mgombea urais chama cha ADC, Wilson Elias akisalimiana na wavuvi wa kisiwa cha Bezi kilichopo mkoani Mwanza alipokwenda kwaajili ya kuomba ridhaa ya chama chake kuongoza nchi. Picha na Saada Amir
Amesema Tanzania itakuwa nchi ya 15 duniani kujiunga na mataifa 14 ambayo tayari yameweka satelaiti kwa ajili ya kudhibiti uhalifu.
Elias, ameeleza kuwa satelaiti hiyo haitaimarisha ulinzi majini pekee, bali pia nchi kavu, na itasaidia mamlaka kuwabaini wahalifu wakiwemo wezi na majambazi kwa urahisi zaidi.
“Utakapolala nyumbani kwako utakuwa na uhakika wa usalama zaidi ya asilimia 100 na hata hawa ndugu zetu polisi watakuwa na kazi ndogo sana ya kuwakamata waharifu, hata wakipelekwa mahakamani kila mharifu ataoneshwa ‘screen’ ataambiwa huyu una mfahamu ambaye ni yeye ndiyo njia pekee tunaenda kukomesha uharifu,” ameeleza.
Amesema Serikali yake haitavumilia vitendo vya uhalifu, na kwamba wananchi watakuwa huru kufanya shughuli zao za kiuchumi usiku na mchana, kwa kuwa jukumu lake kuu litakuwa ni kuwahakikishia ulinzi wa kutosha.
Elias amefafanua kuwa satelaiti hiyo pia itakuwa na uwezo wa kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa, jambo litakalowanufaisha wakulima na wasafiri wa majini.
Aidha, amesema matumizi ya boti za doria katika maziwa yatapunguzwa, na badala yake zitafungwa ‘skrini’ zitakazopokea mawimbi kutoka kwenye satelaiti, yatakayowaonesha wahalifu moja kwa moja ili kurahisisha kuwakamata.
Mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni mgombea ubunge wa Jimbo la Ilemela, Shabani Itutu, amesema watahakikisha wavuvi wanakuwa na benki yao maalumu itakayowasaidia kuendeleza shughuli za uvuvi na biashara zinazohusiana na sekta hiyo.
“Watu wanakopesheka maeneo mengine, lakini mvuvi hakopesheki. Nikiwa mbunge na mheshimiwa Wilson akiwa rais, tunataka kuhakikisha kuna benki maalumu kwa ajili ya wavuvi ili wapate dirisha lao la mikopo, kwa sababu uvuvi umeunganisha watu wengi,” amesema.
Amesema akichaguliwa kuwa mbunge, atahakikisha hakuna mvuvi atakayekamatwa kwa kutumia nyavu zisizofaa, kwa kuwa Serikali ina wajibu wa kuzizuia kabla hazijafika kwa wavuvi.
“Nyavu zisizofaa zilitokaje kiwandani? Ziliendaje dukani? Zililipaje kodi halafu zikaja ziwani mvuvi awe mkosaji? Haitawezekana,” amesema.
Mvuvi, Abel David amesema uvamizi ziwani ni moja ya changamoto kubwa wanazokabiliana nazo na endapo satelaiti hiyo itawekwa, itamaliza kabisa tatizo hilo.
Naye David Mgeta, mvuvi wa eneo la Bezi, amesema wavuvi wanahitaji ulinzi zaidi majini na anaamini teknolojia hiyo ikitekelezwa itawasaidia kuvua kwa amani, bila hofu ya kuvamiwa au kuporwa samaki.
“Ambacho sisi tulikuwa tunaomba akiishapita, rais wetu atatue changamoto za kuvamiwa majini, kuna nyang’anywa samaki, sasa akiisha pita naomba atuwekee ulinzi majini,” amesema Mgeta.
