MGOMBEA UBUNGE CHATO KUSINI ACHANA MISTARI BONGO FREVA AKIOMBA KURA

Mgombea Ubunge Jimbo la Chato kusini,Paschal Lutandula, akichana mistari ya bongo dreva.

…………

CHATO

ZIKIWA zimesalia siku tano kufanyika Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani nchini, mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato kusini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Paschal Lutandula, amelazimika kuchana mistari ya muziki wa kizazi jipya.

Hatua hiyo ililenga kuomba kura kwa wananchi wa kitongoji cha Nyakasiku kilichopo kwenye Kijiji cha Buseresere wilayani Chato mkoani Geita.

Hata hivyo kitendo hicho kimeonekana kuwafurahisha zaidi wananchi wa kitongoji hicho baada ya kumshangilia kwa shangwe kubwa kutokana na kugusa hisia zao za kuibua vipaji kupitia sanaa ya muziki.

Akiwa katika maeneo mbalimbali ya mikutano ya kampeni ndani ya Jimbo hilo, mgombea huyo amekuwa akieleza azma yake ya kukuza uchumi wa Vijana kupitia vipaji vyao huku akiahidi kuandaa tamasha la burudani mbalimbali kila mwaka iwapo atachaguliwa kuwa Mbunge wao.

Aidha amesema ili kutimiza kusudio hilo wananchi hawana budi kumpigia kura nyingi mgombea Urais kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aweze kuchochea maendeleo kwa jamii.

Mbali na hilo, amewaomba kujitokeza kwa wingi Oktoba 29,mwaka huu ili waweze kumpigia kura za Ubunge wa Jimbo hilo pamoja na Diwani wa kata ya Buseresere, Mange Samwel.

Akiwa katika mkutano huo pia amewaahidi kutatua kero ya upatikanaji wa maji safi na salama na kwamba ndani ya siku 100 za Ubunge wake shida hiyo itageuka historia.

Kadhalika amedai atakuwa tayali kuunga mkono ujenzi wa vyumba vya madarasa ya shule ya msingi Nyakasiku ili kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kutafuta elimu.

Kwa upande wake Mgombea udiwani wa Kata hiyo, akalazimika kufikisha kilio cha wananchi wake kwa mgombea Ubunge kutokana na uhaba wa nishati ya umeme kwa wananchi hao.

Vilevile akatumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi hao kuwapigia kura wagombea wanaotokana na CCM ili kutatua kero zao kwa haraka.

                           Mwisho.