Mmisionari wa Kimarekani ametekwa nyara katika mji mkuu wa Niger, Niamey, kwa mujibu wa vyanzo vya usalama na vyombo vya habari vya ndani. Watu watatu wenye silaha waliokuwa kwenye gari aina ya Toyota Corolla walimchukua mwanaume huyo usiku wa kuamkia Jumatano, na inasadikiwa walimtoa nje ya jiji.
Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika, lakini mamlaka za Niger zinashuku kuwa watekaji wanahusiana na kundi la Islamic State. Ripoti za vyombo vya habari vya ndani zinasema Mmarekani huyo ni rubani wa shirika la kimisionari “la Serving in Mission”.
Ubalozi wa Marekani mjini Niamey umethibitisha tukio hilo na kusema unashirikiana na mamlaka za Niger kumtafuta. Serikali ya Marekani imesisitiza kuwa usalama wa raia wake ni kipaumbele cha juu.
Tangu mapinduzi ya kijeshi mwaka 2023, usalama nchini Niger umezorota, huku mashambulizi ya makundi ya kijihadi yakiongezeka. Wataalamu wanasema vitendo vya utekaji nyara vimeanza tena kama njia ya makundi ya wanajihadi kujipatia fedha, hali ambayo inaweza kusababisha mashirika ya misaada ya Magharibi kujiondoa, na hivyo kuongeza umasikini katika eneo la Sahel.
Related
