Mtaalamu wa picha alivyohitimisha ushahidi dhidi ya Lissu

Dar es Salaam. Shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu jana alihitimisha ushahidi wake katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam huku akisisitiza kuwa hawezi kuandika kila kitu kwenye maelezo yake aliyoandika polisi, kwani kwa kufanya hivyo atakuwa anaandika kitabu au ripoti ya utafiti.

‎Shahidi huyo, Mkaguzi wa Jeshi la Polisi, Samweli Eribariki Kaaya (39) ambaye ni mtaalamu wa picha, kutoka Kitengo cha Picha, Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam, alieleza hayo wakati akihitimisha kujibu hoja mbalimbali za kusawazisha ushahidi wake aliyoutoa mahakamani hapo na maswali ya dodoso aliyohojiwa na mshtakiwa Tundu Lissu.

Shahidi huyo ametoa ushahidi huo kwa siku sita mfululizo kuanzia Jumatano Oktoba 15 hadi Oktoba 23 alipohitimisha.

Alikuwa mbele ya majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo, Dunstan Ndunguru, James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi (SSA), Tawab Issa, kujibu swali moja la kusawazisha majibu aliyoyatoa kwenye maswali ya dodoso aliyohojiwa na Lissu, Kaaya alisema maelezo yake ya maandishi aliyoyaandika Polisi ni muhtasari tu wa kile alichokifanya na kwamba asingeweza kuandika kila kitu kwenye maelezo hayo kwa kuwa hayo yasingekuwa maelezo ya ushahidi, bali ingekuwa ripoti ya utafiti au kitabu.

Kaaya alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa na Lissu maswali katika maeneo 75 yanayohusu maelezo yake ya ushahidi wa mdomo mahakamani, ambayo hayako kwenye maelezo ya maandishi aliyoyatoa polisi.

Katika majibu yake kwa baadhi ya maswali Kaaya akikiri kuwa anafahamu na kwenye nyingine aliijibu kuwa hafahamu,kama ifuatavyo:

Lissu: Shahidi unafahamu umeulizwa maswali 165 hapa mahakamani na mawakili wa Jamhuri?

Lissu: Unafahamu kati ya maswali hayo 165 uliyoulizwa na mawakili wako, maswali 112 hayapo kwenye maelezo yako uliyoandika polisi?

Lissu: Shahidi, asilimia 68 ya maswali uliyoulizwa na wakili wa Serikali hayapo kwenye maelezo yako uliyoandika Polisi, ni kweli au si kweli?

Lissu: Kwa nini maelezo ya ushahidi wako uliyoyatoa hapa mahakamani hayapo kwenye maelezo uliyoandika Polisi?

Shahidi: Maelezo niliyoandika polisi ni summary (muhutasari) wa kile nilichokifanyia kazi, huwezi kuandika kila kitu kwa sababu utakuwa unaandika research (utafiti).

Lissu: Umetoa sababu hapa mahakamani kwa nini hukuandika maelezo ya ushahidi ulioutoa mahakamani?

Lissu: Nani ameandika hayo maelezo yako Polisi?

Shahidi: Nimeandika mimi.

Lissu: Katika maelezo uliyoandika, nani alikukanya (kukuonya)?

Shahidi: Maelezo ya onyo hayana kukanya.

Lissu: Nani aliyekukanya?

Shahidi: Niliandika mwenyewe.

Lissu: Kwenye kuandika maelezo polisi huwa kuna uthibitisho, kweli au si kweli?

Shahidi: Niliandika mimi.

Lissu: Nani aliyewafundisha nyie mapolisi kuandika maelezo ya onyo.

Shahidi: Mapolisi wenzetu.

Lissu: Shahidi, unafahanu Polisi General Order ( PGO)?

Lissu: Mara ya mwisho kusoma hiyo Polisi General Order ni lini?

Lissu: Shahidi, mimi hapa ninakabiliwa na kesi ya uhaini, ninatuhumiwa mimi ndio niliyerusha matangazo mubashara katika mkutano wangu na kuyaingiza mtandaoni, sasa waeleze majaji, inawezekana mtu huyo huyo anaongea na huyo huyo ameshikilia kamera anarekodi mubashara na wakati huohuo anaongea?

Lissu: Shahidi, katika uchunguzi wa kitaalamu unaweza kujua ni nani aliyeweka hiyo video mtandao, maana mimi ndio natuhumiwa nimeiweka hiyo video mtandaoni.

Shahidi: Unapofanya uchunguzi wa metadata unaangalia link iliyopandisha hiyo video, hivyo mimi sikubaini mtu.

Lissu: Umejibu vizuri sana shahidi na Mungu akubariki.

Lissu: Waeleze majaji nani alikuwa anatumia hiyo kamera siku ya Aprili 3, 2025 kwa ajili ya kurekodi.

Shahidi: Sijui na wala simfahamu.

Lissu: Kwa ufahamu wako, inawezekana mtu ambaye hana username ya Jambo TV, hana akaunti ya Youtube, password, siyo mfanyakazi wa Jambo TV, inawezekana kwa mtu asiye na uhusiano wa namna hiyo akaweka video Jambo TV?

Shahidi: Inategemea na sasa teknolojia imekuwa kuna kitu kinaitwa hacks (udukuzi), ambacho mtu anaweza kuingia kwenye akaunti ya mtu bila password (nywila).

Lissu: Shahidi, hayo yote uliyosema nimevutiwa nayo, lakini hapa nina tuhuma kuwa mimi ndio nimetoa maeneo ya uhaini na kuyaingiza kwenye akaunti hiyo, hebu naomba kupata uelewa kwenye hilo.

Shahidi: Hakuna namna mtu anaweza kuingia kwenye akaunti, labda awe na password na kama hana kama una kitu kinaitwa software ya kuvunja na kuingia kwenye akaunti ya mtu bila kuwa na password na kuingia au mtu anaweza ku-hack (kudukua) akaunti.