NDANI ya ofisi hiyo, afisa aliyefuatana naye ambaye alijitambulisha kwake kwa jina la Aidan alimkabidhi Muddy kila kitu alichokuwa amekikabidhi kwa maafisa uhamiaji waliomkamata.
Muddy aliviangalia vitu alivyokabidhiwa, kila kitu kilikuwepo kasoro kitu kimoja tu ambacho hakuwa amekiona.
Wakati akiendelea kupekua vitu vyake, Aidan alimtaka Muddy amfuate hadi katika chumba kingine na walipofika katika chumba hicho, afasi yule wa uhamiaji alimuacha Muddy humo naye akaondoka zake.
Katika chumba hicho kulikuwa na kochi moja tu na hakukuwa na kitu kingine wala mtu yeyote.
Kilikuwa chumba kikubwa kilichokuwa na madirisha ya vioo, ndani yake taa zilikuwa zinawaka muda wote na viyoyozi vilikuwa vikipuliza kwa mbali.
“Bon Voyage… (safari njema)” kabla ya kutoka nje Aidan alimtamkia Muddy na kuzidi kumkatisha tamaa ya matarajio yake.
Hata hivyo, Muddy hakuweza kuitikia salam huyo iliyomtia simanzi na uchungu kutoka kwa Aidan. Maneno hayo yalibeba ujumbe mzito wenye maumivu makali moyoni mwake. Yalikuwa maneno makali na machungu kama msumali wa moto uliopigiliwa utosini mwake.
Tayari alishajua kila kitu kilikuwa kimeharibika, hapo aliutumia muda huo kuvikagua vitu vyake alivyokabidhiwa na Aidan, na alipata uhakika wa kutokuwepo kwa hati yake ya kusafiria.
Kutokuwapo kwa hati hiyo kulimfanya aamini ilikuwa bado ikishikiriwa na maafisa hao na wangeweza kumkabidhi wakati atakapkuwa akipandishwa ndege kurudishwa Tanzania.
***
Muddy alijiinamia na machozi yaliendelea kumchuruzika kama mtu aliyekuwa amepewa taarifa ya msiba.
Tangu alipoachwa katika chumba hicho na Aidan, zilipita dakika kumi na tano akiwa ameketi kinyonge katika kochi pekee alilolikuta ndani ya chumba hicho.
Kuna fikra nyingine zikamuingia akilini mwake, Muddy alijiona kama alikuwa huru kuweza kufanya jambo ambalo lingeweza kuwa na manufaa kwa maisha yake ya baadaye.
Kuna kitu aligundua hakikuwa sawa, alibaini hakukuwa na ulinzi wowote uliokuwa ukimfuatilia akiwa ndani ya chumba hicho, hivyo akafikiria kama angeweza kutoroka katika eneo hilo na kutokomea na kwenda kujichanya mitaani katika mji huo wa Stockhom.
Mawazo yake yalimwambia angeweza kuanza maisha mapya katika jiji hilo kama angefanikiwa kutoka salama ndani ya uwanja huo wa ndege wa Arlanda.
Wakati akilipokuwa akifikiria hayo, alijaribu kuangaza kila upande wa chumba hicho na kudhani labda angeweza kuona nje lakini kila upande ulioutazama kulikuwa na kioo ambacho kilikuwa kikimuonesha taswira yake.
Alijifuta machozi, kisha akasogea hadi katika mlango alioingilia na kuujaribu kuufungua, kitu kilichomshangaza mlango ulitii amri na kuwa wazi, alichungulia nje na kuwaona watu wakiwa wanaendelea na pilikapilika zao.
Wazo la kutaka kutoroka likaendelea kujijenga akilini mwake, lakini kuna kitu kikagonga akilini mwake, wasiwasi ukamkumba na kujikuta akikosa utulivu wa akili.
Hofu ilikuwa imemuingia, ni kama kulikuwa na kitu kilichokuwa kimemtisha, Muddy hakuwa akizijua njia za kutokea ndani ya uwanja huo wa ndege.
Hakujua mwelekeo wake kama angefanikiwa kutoka ndani ya chumba alichokuwamo.
Suala la kutojua njia ya kuifuata baada ya kutoka hapo, lilimfanya kuwa mlemavu wa macho ingawaje alikuwa na macho yake mawili.
Kitu kingine alichokuwa akikifikiria ni kwamba labda katika chumba hicho kulikuwa na uwezekano wa kutegeshwa kamera za siri ambazo zilikuwa zikimfuatilia.
“Wazungu si wajinga waniache tu hivihivi bila ya uangalizi wowote…” aliwaza.
Muddy aliamini laiti angejaribu kutoroka kwa kutoka ndani ya chumba hicho, asingeweza kufika mbali, angekamatwa kama mtoto mdogo anayejifunza kutambaa.
Mara alipofikiria hivyo unyonge ukamuingia, akarudi kwenye kochi na kuketi huku akisubiri hatima yake ya kurudishwa Tanzania.
Tayari alishakubaliana na matokeo… hata yale maombi ya kuomuomba Mungu alishayaacha.
***
Zilipita kama dakika ishirini tangu aliporudi kuketi kwenye kochi, wakati akiwa ameshakata tamaa na kuuondoa akilini mwake mpango wa kutaka kutoroka na kukubaliana na chochote ambacho kingetokea, ghafla mlango wa chumba alichokuwamo ulifunguliwa na mtu mmoja aliingia na kusimama mbele yake.
Muddy akiwa katika hali ambayo hakuifahamu naye alijikuta akiinuka kutoka kwenye kochi alilokuwa ameketi na kusimama kama vile aliyeamrishwa kufanya hivyo baada ya kumuona mtu aliyeingia. Mtu huyo alikuwa mwenye uso maridadi wenye mviringo kama umbile la moyo wa binadamu.
Macho yake ya rangi ya bluu na nywele zake ndefu za dhahabu zilizosokotwa na kufungwa kwa umaridadi nyuma ya kisogo chake.
Midomo yake iliyochongwa vizuri na mashavu yaliyojaa kwa kiasi kama mkate wa kumimina uliopikwa na mpishi wa Kitanga. Mtu huyo alikuwa na ngozi yenye mng’ao wa asili iliyosheeni rangi yenye mwanga laini na yenye afya.
Kimo chake usingeweza kusema ni mfupi wala usingempa sifa ya urefu, alikuwa wa saizi ya kati, kama haitoshi, alikuwa amevaa suruali yenye rangi bluu ya giza, fulana nyepesi yenye rangi ya samawati, chuchu zake zenye ukubwa wa embe sindano zilichomoza kama zilitaka kuipasua fulana yake.
Chini alikuwa na viatu vyeusi aina ya buti. Mara baada ya Muddy kumuona mtu huyo uso wake ulichanua na kuachia tabasamu jepesi huku akiamini alikuwa kwenye mikono salama.
Furaha ilikuwa imechanua usoni pake. Kwa dakika kadhaa alikuwa amesahau mateso na tabu zote alizokuwa akizifikiria akilini mwake…
Muddy ni kama alikuwa kama amemuona malaika wa heri akiwa amechanua mbawa zake mbele yake… Mtu huyo hakuwa mwengine zaidi ya Linnie Jonson.
“Finally we have met once again. (Hatimaye tumeonana kwa mara nyingine)” Linnie alisema na kuachia tabasamu lililoonyesha meno yake meupe yalipangiliwa vizuri kinywani mwake.
“God is great…” (Mungu ni mkubwa), Muddy ilikuwa zamu ya Muddy kushukuru huku furaha ya matumaini ikirejea ndani ya nafsi yake.
Katika mazingira yaliyozidi kumjengea imani ya kuendelea na safari yake, Muddy alimshuhudia Linnie akimsogelea na kuchanua mikono yake kuashiria kwamba alikuwa akitaka kumkumbatia.
Naye bila ya kukitafakari kitendo hicho… akajikuta akimfuata pale alipokuwa amesimama, wakakumbatiana na kila mmoja akionesha kutawaliwa na furaha… hali iliyomzidishia faraja na matumaini makubwa na kuamini Linnie amemtengenezea mizingira ya kuendelea na safari yake ya Uholanzi.
Mgusano wao ulizua msisimko wa hisia za aina yake, uliusisimua miili ya kila mmoja wao, kuonesha kwamba upendo ulikuwa umetawala kati yao.
Ilikuwa faraja kubwa kwa Muddy kukumbatiana na Linnei na kuweza kuvutiwa na manukato yake. Mwanamke huo alikuwa amepaka manukato ya kuvutia na kuzifanya pua za Muddy zivute hewa safi iliyokuwa imechanganyika na manukato hayo.
Hakika alijisikia kuwa katika mikono salama na yenye amani. Nafsi yake ilifarijika zaidi kukutana na mwanamke huyo.
Hatimaye Linnie alimuomba, Muddy kurudi kuketi kwenye kochi, naye akaketi karibu yake kisha kwa mara nyingine tena akataka amwambie ukweli undani wa maisha yake.
“What were you after in Amsterdam? (Ulikuwa unafuata nini Amsterdam?)” Linnie alimuuliza Muddy kwa kiingereza kizuri.
Muddy hakutaka kuficha kitu, alimwambia mwanamke huyo kila kitu kuhusu maisha yake ya Tanzania na kuuzungumzia umasikini uliokuwa umetawala katika familia yao.
“I have come to seek a better life. (Nimekuja kutafuta maisha bora),” alijibu kwa aibu huku akijaribu kueleza changamoto za maisha ya aliyoyakimbia Tanzania.
“Were you really going to school…? (Ni kweli ulikuwa ukienda masomoni…?)”
“No, it was a way to go and find a life in the Netherlands…(Hapana, ilikuwa ni njia ya kwenda kutafuta maisha Uholanzi…)” Muddy alifunguka ukweli mbele ya mwanamke huyo mbichi akiamini angeweza kumsaidia na kumtengenezea mazingira ya kuendelea na safari yake.
“ Because you have to find a life in Amsterdam or you can live anywhere in Europe. (Kwani ni lazima utafute maisha Amsterdam au unaweza kuishi sehemu yoyote ya Ulaya?)” Linnie alimuuliza swali hilo huku akimkazia macho Muddy.
Baada ya kutafakari kwa sekunde chache, Muddy alimwambia Linnie kwamba angeweza kuishi sehemu yoyote ya Ulaya na sio lazima aende Amsterdam ili mradi apate kazi ya kuyaendesha maiksha yake.
“ Are you ready to live in Sweden? (Uko tayari kushi Sweden?)”
“Y es, I’m ready. (Yaa, niko tayari,” alijibu Muddy bila ya kuijua dhamira aliyokuwa nayo Linnie katika kumuuliza swali hilo.
***
Baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati yao, hatimaye Linnie aliitoa hati ya kusafiria ya Muddy na kumuonesha alikuwa amemuombea kibali cha kuishi Sweden kwa miezi mitatu.
“If you behave well, you will be given another period to live in Sweden…(Kama utakuwa na mwenendo mzuri, utaongezewa muda mwingine wa kuishi hapa Sweden…).”
“Thank you for that…” (Nashukuru kwa hilo…)” alijibu kwa unyenyekevu.
Awali Muddy hakuamini alichokuwa akikisikia kutoka katika kinywa cha Linnie na kukiona kwenye hati yake ya kusafiria, hakuamini kama Linnie angeweza kufanya kile alichokuwa amekifanya.
Machozi ya furaha yalimmwagika usoni pake na kujihisi ni mmoja kati ya watu wenye bahati kubwa sana duniani.
Mtoto wa Mjini – 12