Ngorongoro yalenga kukusanya Sh350 bilioni kwa mwaka 2025/2026

Arusha. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imejiwekeza malengo ya kukusanya zaidi ya Sh350 bilioni katika mwaka wa fedha 2025/2026 kutoka katika vyanzo vyake vya mapato ikiwemo utalii na utoaji wa huduma.

Malengo hayo mapya yanakuja baada ya mamlaka hiyo kufanikiwa kuvuka lengo lake la makusanyo kwa mwaka wa fedha uliopita (2024/2025), ambapo ilikusanya jumla ya Sh269.9 bilioni, ikiwa ni ongezeko la Sh230 bilioni ya malengo waliyokuwa wamejiwekea.

Akizungumza kwenye hafla ya kuwavisha cheo makamishna wawili wasaidizi waandamizi wa uhifadhi leo, Oktoba 24, 2025, jijini Arusha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NCAA, Jenerali Venance Mabeyo, amesema kuwa malengo hayo ni kuhakikisha mamlaka inakusanya fedha za kutosha kusaidia Serikali kuhudumia wananchi wake.

Mabeyo, ambaye ni Mkuu wa Majeshi mstaafu, amesema kuwa makamishna wasaidizi waandamizi wa uhifadhi ni injini ya Ngorongoro katika kutimiza malengo yake.

Amewataka kuhakikisha wanasimamia idara walizopewa kwa kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu za taasisi, ili kuleta tija.

“Niwaambie tu wazi, kwa mwaka huu wa fedha tunalenga kukusanya zaidi ya Sh350 bilioni kutoka bilioni 269 tulizokusanya mwaka huu, sasa hili haliwezi kutimia bila nyie kutimiza majukumu yenu ipasanyo,” amesema.

“Hivyo, nendeni mkasimamie mapato na matumizi ya taasisi, lakini pia mkawe wabunifu wa vyanzo vipya vya mapato ikiwemo kubuni mazao mapya ya utalii ili angalau tufikie malego na tuvuke,” amesema.

Amesema kuwa kwa kufanya hivyo watasaidia Serikali kupata fedha za kuhudumia wananchi katika kutatua changamoto mbalimbali za kwenye jamii wanazokumbana nazo ikiwemo huduma za afya, umeme, maji na elim.

“Mfano mzuri kuna mapango ya Amboni kule Tanga na Kimondo kilichoko Songwe, hizi zikiboreshwa vizuri na kuwekewa miundo mbinu bora inaweza kuvuta watalii wengi na kuongeza mapato,” amesema.

Mbali na hilo amewataka kusimamia vizuri idara ya Tehama ili kuhakikisha mifumo ya NCAA inafanya kazi kwa viwango vya kimataifa ikiwemo kusaidia kutoa huduma kwa watalii lakini pia  kutoa taarifa haraka za upotoshaji wowote unaoibuliwa dhidi ya mamlaka hiyo.

“Eneo lingine ni eneo la Tehama ambalo Mamlaka inapitia katika kipindi cha mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia, hivyo ni jukumu sasa la kusimamia idara vizuri kuhakikisha teknolojia ya habari na mawasiliano inafanya kazi kwa viwango vya kimataifa ili kuwawezesha watalii wetu kutoka nchi mbalimbali duniani waweze kutumia kuhakikisha wanapata huduma bora.

“Lakini pia tumeona upotoshaji mwingi katika eneo la Ngorongoro na dunia inapotosha na hii ni nafasi yetu kuhakikisha taarifa zetu zinawafikia watu ambazo ni sahihi na  kwa wakati ili upotoshaji utakaoibuka au unaoendelea usiendele kuharibia sifa eneo letu tunalotegemea kwa mapato,” amesema.

Waliovishwa cheo baada ya kuhitimu mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Brown Shimwela, anayesimamia Idara ya Fedha, pamoja na Kamishna Msaidizi Mwandamizi Dk Amani Makota, anayesimamia Idara ya Tehama na Takwimu.

Awali, Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Abdul-Razaq Badru, amesema kuwa makamishna hao wapya wanajiunga na Menejimenti ya Ngorongoro kuongeza nguvu kazi katika utekelezaji wa majukumu ya kusimamia uhifadhi, utalii, na maendeleo ya jamii, kwa lengo la kukuza uchumi wa taifa kikamilifu.

Badru ametumia nafasi hiyo kuwataka viongozi hao wapya kushirikiana na Menejimenti ya Ngorongoro kuboresha miundombinu ya utalii, huduma kwa wateja, kubuni mazao mapya ya utalii, na kusimamia kikamilifu maeneo ya malikale yaliyopo nje ya eneo la Ngorongoro ili kuongeza mchango wa utalii katika pato la taifa.

Kwa upande wake, Dk Makota amesema anamshukuru Mungu kwa kufanikishwa kuhitimu na kuvishwa cheo hicho cha kusimamia kitengo cha Tehama, na kuahidi kuleta mabadiliko makubwa.

“Tunakwenda kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika kitengo cha Tehama, hasa kuhakikisha mifumo inasomana na taasisi zingine.

Pia, tutahakikisha tunaboresha mifumo yetu ya ndani ili kutoa huduma bora kwa wateja kutoka mataifa mbalimbali, hivyo tegemeeni mambo makubwa,” amesema Dk Makota.