Dar na Pwani. Wakati baadhi ya wenyeviti wa Serikali za mitaa wakijitosa kuwania udiwani kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imesema wale watakaochaguliwa kuwa madiwani watalazimika kung’atuka kwenye nafasi za awali.
Wenyeviti hao ni wale waliochaguliwa kwenye uchaguzi uliopita wa Serikali za mitaa uliofanyika mwaka 2024.
Baadhi ya wenyeviti wa mitaa katika wilaya kadhaa za Dar es Salaam na Pwani wamejitosa kuwania udiwani, jambo ambalo limeibua sintofahamu kwa wananchi wa mitaa yao endapo watachaguliwa kuwa madiwani, wataendelea na nyadhifa mbili za kuchaguliwa na wananchi kwa wakati mmoja?.
Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Mitaa) G.N. No. 283 ya mwaka 2019, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ni kiongozi wa mtaa, anayechaguliwa na wananchi wa mtaa husika na kazi yake ni kusimamia utendaji wa Serikali ya Mtaa, kuongoza mikutano ya mtaa, na kutekeleza maelekezo ya Halmashauri kupitia Afisa Mtendaji wa Mtaa.
Wakati Diwani ni mjumbe wa baraza la Halmashauri (Manispaa, Jiji, au Wilaya), anayewakilisha kata nzima, akihudhuria vikao vya baraza, anapitisha maamuzi na bajeti za halmashauri, ana wajibu wa usimamizi wa maendeleo ya kata nzima ambayo inaweza kuwa na mitaa kadhaa au vijiji.
Hata hivyo sintofahamu kwa wananchi imekuja kipindi ambacho baadhi ya wagombea wa udiwani kwenye baadhi ya wilaya za Dar es Salaam na Pwani ni wenyeviti wa Serikali za mitaa wakihoji ni vipi wanaweza kushika nyadhifa zote mbili?
“Lazima kutakuwa na mgongano wa maslahi, mtaa uko chini ya kata, hivyo diwani hawezi kuwa anasimamia mtaa ambao yeye mwenyewe ni mwenyekiti wake, lazima kuna vitu vitakuwa haziendi sawa,” amesema Neema Jonas wa Kibaha.
Elinaza Kuke wa Temeke amesema imewahi kutokea mwenyekiti wa mtaa wao alichaguliwa kuwa diwani kwenye chaguzi zilizopita na alisalia na vyeo vyote viwili kwa wakati mmoja.
Akifafanua hilo, Katibu Mkuu wa Tamisemi, Adolf Ndunguru amesema ni kosa kisheria mtu mmoja kuwa na nafasi mbili za kuchaguliwa na wananchi kwa wakati mmoja.
Amesema inapotokea mwenyekiti wa Serikali za Mitaa amechaguliwa kuwa diwani basi anajiuzulu nafasi ya mwenyekiti wa mtaa.
“Ni kama mtu anapokuwa kazini, akiomba kazi nyingine na kupata anaacha ile ya awali, vivyo hivyo kwa hawa, si kosa mwenyekiti wa Serikali za mitaa kugombea udiwani. Lakini anapotangazwa kuwa mshindi, anapaswa kuachia nafasi moja,” amesema Ndunguru.
Akizungumzia wenyeviti waliojitosa kwenye udiwani katika uchaguzi wa mwaka huu, Ndunguru amesema bado hawajapata taarifa hizo, lakini kama wapo na wakashinda udiwani, basi ile mitaa waliyokuwa wakiiongoza itafanya uchaguzi mdogo kupata mwenyekiti mwingine.
Wakizungumza na Mwananchi leo Oktoba 23, 2025 baadhi ya waliokuwa wenyeviti wa Serikali za Mitaa walioomba hifadhi ya majina yao wamesema hawatakuwa na sababu ya kuendelea na nafasi za awali, endapo watachaguliwa kwenye udiwani.
“Binafsi nilijipima nikajiona Natosha kugombea udiwani baada ya kuwa kwenye nafasi ya mwenyekiti kwa vipindi viwili, nikipewa ridhaa na wananchi wa kata yangu, basi kwenye mtaa nitaachia wengine,” amesema.
Mwenyekiti mwingine aliyejitosa kugombea udiwani amesema mwaka jana wakati wa uchaguzi wa mitaa aligombea kwa kuwa aliongoza nafasi hiyo kwa mafaniki na mwaka huu wananchi wake wakamshawishi agombee udiwani kwa kuwa ana sifa.
“Sikuwa na nia ya kugombea udiwani, lakini uwezo na namna nilivyowatumikia wananchi, wakanishawishi nipande kwenye udiwani, nikipewa ridhaa basi nitachia wengine wavae ‘viatu’ vyangu kwenye uenyekiti,” amesema.
Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288 (Revised Edition 2002) Kifungu cha 60(2) kinasema mwenyekiti wa serikali ya mtaa hawezi kuwa diwani kwa wakati mmoja.
Mwenyekiti wa mtaa akichaguliwa kuwa diwani, mara tu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi au TAMISEMI inapothibitisha, anafutwa kuwa mwenyekiti wa mtaa mara moja Kwa mujibu wa Kanuni ya 8(1)(c) ya G.N. No. 283/2019 na kifungu cha 60(2) cha Cap. 288, mtu anayeshika nafasi ya kuchaguliwa ya ngazi ya juu (udiwani) anapoteza sifa ya kuendelea na nafasi ya chini (mtaa).
Afisa Mtendaji wa Mtaa (Executive Officer) atatuma taarifa kwa Mkurugenzi wa Manispaa au Halmashauri, kuthibitisha kuwa nafasi hiyo imekuwa wazi kwa mujibu wa Kanuni ya 22(1) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Mitaa), G.N. No. 283 ya 2019):l inayosema
Iwapo nafasi ya mwenyekiti wa mtaa itakuwa wazi kwa sababu ya kifo, kujiuzulu au kupoteza sifa, uchaguzi mdogo utafanyika kwa mujibu wa kanuni hizi.
Baada ya mtaa kupoteza mwenyekiti, unatangazwa uchaguzi mdogo wa mwenyekiti wa mtaa, Wananchi wa mtaa huo wanachagua mwenyekiti mpya kupitia utaratibu uleule wa kawaida wa mgombea, kampeni, kura na matokeo.
Wakati huo mjumbe wa Kamati ya Mtaa (anayechaguliwa na wajumbe wengine) anaweza kuteuliwa kuwa kaimu mwenyekiti (Acting Chairperson) kwa muda, hadi uchaguzi mdogo ukamilike kwa mujibu wa Kanuni ya 23(2) ya G.N. 283/2019..
