Zanzibar. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan, amesema wataulinda Muungano kwa nguvu zote kwani una faida kwa pande zote mbili (Bara na Visiwani) huku akieleza chama hicho kikipewa ridhaa wataendeleza uchumi mkubwa na maendeleo jumuishi.
Nyingine ni maendeleo jumuishi yanayomchukua kila Mtanzania na kuwa wataenda kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha huduma za kijamii ikiwemo elimu, maji, afya elimu pamoja na umeme unamfikia kila mtu na kuwa changamoto ya umeme Zanzibar watasimama imara kumaliza kadhia hiyo ili huduma hiyo ipatikane saa 24.
Samia ameyasema hayo na mengine yaliyopo kwenye ilani ya CCM ya 2025/30, leo Ijumaa Oktoba 24,2025 akizungumza wakati wa kufunga kampeni kwa upande wa Muungano, kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Mkoa wa Magharibi, Zanzibar.
Mgombea huyo ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema kuwa wataenda kuulinda Muungano kwa nguvu zote kwani Muungano una faida kwa pande zote.
Samia amesema Serikali za CCM (Muungano na Zanzibar) zinathamini utekelezaji wa ahadi zinazotolewa na chama hicho na kuwa katika ilani inayoisha ya 2020/24 kazi kubwa imefanyika.
“Kuhusu maendeleo jumuishi yanayomchukua kila mtu, kila Mtanzania, tutaenda kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha hduma za jamii elimu, maji, afya elimu na umeme unamfikia kila mtu.
“Natambua kwa sasa tuna changamoto kidogo ya umeme Zanzibar, tumesimama imara kumaliza kadhia hii mimi na Mwinyi (Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi) na umeme utakuwa unawaka saa 24,” amesema.
Mgombea huyo akizungumzia uwezeshaji wananchi kiuchumi ameahidi wataendelea kutoa mitaji na fursa za kufanya biashara na kuwa wataweka nguvu kubwa ili vijana wajiajiri na kuendesha maisha yao.
“Katika kukuza uchumi mkubwa, pande zote mbili za Muungano tunafanya kazi kwa pamoja kukuza uchumi wetu mkubwa wa nchi na katika hili tumefanya kazi kubwa kuhakikisha vichocheo vya uchumi tunaimarisha ikiwemo usafiri na usafirishaji amnao ukikaa vizuri tutaimarisha biashara na uchumi.
“Sekta za uzalishaji na hapa Zanzibar sekta za uchumi wa buluu, viwanda na kilimo na tunaenda kuvalia njuga tuhakikishe tunafanya vizuri. Kwenye sekta za uchumi tunaenda kukalia kidete ili tujenge uchumi mkubwa. Zanziba uchumi wa buluu, mafuta na uvuvi wa bahari kuu ni maeneo ambayo yanatupa mwanga huko mbele kwa ajira ya vijana wetu na tutaenda kufanyia kazi,” amesema.
Awali, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi, amewataka wananchi kujitokeza Oktoba 29,2025 kupiga kura na kuchagua CCM.
“Tumezifanya kwa ustaarabu mkubwa watu wengi na makundi maalumu tuna imani kote huko tulipopita wananchi watatuchagua kwa kishindo nasi hatuna sababu ya kutoamini hilo. Kampeni ni moja na kupiga kura ni suala lingine niwaombe wananchi mjitokeze kupiga kura, nimuombee kura Samia, mimi mwenyewe na wawakilishi,” amehitimisha.
Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, amesema uchaguzi ni tukio la hesabu za kura na kuwataka Watanzania kulinda Muungano kwa kujitokeza kwa wingi kukichagua chama hicho.
“Naamini CCM tutakuwa na kura nyingi na tutashinda. Nathibitisha maneno yangu haya kwa vuguvugu nililioliona la kampeni Bara na Zanzibar, wingi wa wana CCM na wananchi naamini kwa mahudhurio yale yanafanya ushindi wetu hauna shaka,” amesema na kuongeza;
“Lazima twende tukapige kura tuzingatie misingi ya amani, utulivu, umoja na mshikamano na tukishapiga kura wananchi kila mmoja wetu arudi nyumbani akapumzike angoje matokeo hizo ndiyo nasaha zangu kubwa kwenu, tusiranderande mitaani, tusifanye bughudha na chuki hayo ni mambo ya kishetani CCM hatuna mambo hayo,” amesema.
Akizungumzia Muungano, Dk Shein amewapongeza Samia na Dk Mwinyi kwa kuendelea kuimarisha Muungano na kuwa Muungano ni hazina licha ya kuwa kuna wanaouvizia ili wauvunje.
“Muungano wetu ndiyo hazina yetu watu wanauvizia huu Muungano wanatamani wauvunje, lakini hawawezi sisi tutautunza Muungano kwa kuchagua CCM. Tunapochagua kulinda Muungano wetu tunathibitisha uiamra wa mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, tuyalinde, tuyaendeleze, tuyalinde na tuyadumishe kwani hatuna mbadala wa Muungano, tulinde amani ya nchi yetu,” amesisitiza.
