Serikali yagawa pikipiki kwa maofisa maendeleo ili kuongeza ufanisi

Songwe. Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu imekabidhi pikipiki nane kwa maofisa maendeleo ya jamii wa Mkoa wa Songwe ili kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Maofisa Maendeleo ya Jamii kutoka halmashauri nne kati ya tano za mkoa huo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki hizo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Felesiter Mdemu amesema pikipiki hizo nane zilizogawiwa ni kati ya 98 ambazo serikali imenunua kwa ajili ya kugawa kwa maofisa maendeeo ya jamii nchini ili kuwarahisishia utendaji kazi.

Amesema pikipiki hizo zimetolewa kwa watumishi hao ikiwa ni mpango wa Serikali nchini kuhakikisha inatatua changamoto inayowakabili ya kushindwa kufika maeneo ya vijijini kutatua changamoto na kutoa elimu kwa wananchi.

“Serikali imewapatia nyenzo hizo muhimu ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yenu, hivyo fanyeni kazi kwa bidii, uadilifu na kujituma zaidi kuhakikisha mnawafikia wananchi kwa wakati tofauti na awali,” amesema Mdemu.

Mdemu amesema lengo kuu la kugawa pikipiki hizo ni kutambua thamani ya mchango wa maofisa hao katika jamii, sambamba na kurahisisha kazi za ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, masuala ya ustawi wa jamii na huduma kwa makundi maalumu kama wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu.

“Tunataka kuona matokeo chanya ya uwezeshaji huu, pikipiki hizi ziwasaidie kufika mbali zaidi, kufuatilia miradi kwa karibu na kuwahudumia wananchi ipasavyo kwani matarajio ya serikali inatarajia mtaongeza uwajibikaji na ubunifu katika kazi zenu,” amesisitiza Mdemu.

Amesema pikipiki hizi ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuwawezesha watumishi wa umma kufanya kazi zao kwa ufanisi huku ikitambua mchango mkubwa wa Maofisa Maendeleo ya Jamii katika kuwafikia wananchi na kuratibu shughuli za maendeleo, hasa katika maeneo ya vijijini.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, John Mwaijulu amesema uwezeshaji huo utasaidia kupunguza changamoto ya usafiri iliyokuwa inawakabili Maofisa Maendeleo ya Jamii kwa muda mrefu, jambo lililokuwa likichelewesha utekelezaji wa baadhi ya majukumu yao.

“Mpaka sasa Serikali kupitia wizara hiyo imetoa pikipiki 12 kwa Mkoa wa Songwe ambapo awali zilitolewa pikipiki 4 na sasa pikipiki nane hali ambayo itaongeza ufanisi wa kazi kwa watumishi hao waliopo ngazi ya vijiji na kata,” amesema Mwaijulu.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa pikipiki afisa maendeleo ya jamii Wilaya ya Mbozi, Nelisa Paulo ukosefu wa vyombo vya usafiri ni changamoto iliyokuwa inakwamisha utendaji kazi ikiwepo kufuatilia urejeshwa wa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

“Tulikuwa tunashundwa kuwafikia wananchi vijijini kuwapa elimu ya mikopo, ufuatiliaji wa marejesho ya fedha za mikopo, ujio wa pikipiki hizo utarahisisha utendaji kazi vizuri,” amesema Nelisa.

Ofisa Maendeleo Wilaya ya Momba, Jacobo Mwankemwa ameishukuru Serikali kuwagawia pikipiki hizo ambazo zitawawezesha kuwafikia kwa wakati na urahisi wananchi katika maeneo mbaimbali ya vijijini kuwahudumia.