MCHEZO wa mpira wa miguu umekuwa na stori nyingi sana zinazowahusu wachezaji, makocha, mashabiki na hata wamiliki wa timu. Pengine si mara moja umewahi kusikia mchezaji anabadilisha nafasi ya kucheza uwanjani, lakini kila mmoja amekuwa na stori yake ya tofauti.
Pale kwenye kikosi cha Mafunzo kinachoshiriki Ligi Kuu Zanzibar, kuna kipa anaitwa Shomari Mbwana. Amezungumza na Mwanaspoti akisimulia mambo kadhaa ikiwamo namna alivyobadilika kutoka beki hadi kuwa kipa.
Mbwana ni kati ya wachezaji waliofanya vizuri msimu uliopita wa Ligi Kuu Zanzibar 2024-25 ambao ulifanya wachezaji wengi kupata nafasi ya kutua Tanzania Bara kucheza soka, lakini yeye ameendelea kubaki huko.
Miongoni mwa wachezaji waliotoka Ligi Kuu Zanzibar na kutua Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-26 ni Abubakar Nizar Othman ‘Ninju’ (JKU) na Abdulnasir Abdallah ‘Casemiro’ (Mlandege) waliotua Yanga. Wengine ni Abdallah Iddi Pina kutoka Mlandege ametua Pamba Jiji, Ali Salehe Machupa na Suleiman Said Abraham waliotoka KVZ na kutua Namungo. Wakati hao wakipata nafasi, wapo ambao wanaendelea kusikilizia huenda siku moja nao watafikia malengo hayo, miongoni mwao ni kipa wa Mafunzo, Shomari Mbwana.
Mbwana ambaye msimu uliopita 2024-25 alikuwa akiitumikia Junguni United kwa mkopo, sasa amerejea Mafunzo kuendelea kupambania nafasi na malengo yake.
Kipa huyo ambaye msimu wa 2024-25 alicheza mechi 26 kati ya 30 za Ligi Kuu Zanzibar akiwa na Junguni, aliisaidia timu hiyo kuepuka kushuka daraja ikimaliza katika nafasi ya 11 ikivuna pointi 40, huku yeye akiwa na cleansheet 10. Pia Oktoba 2024 alitwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi.
Mbwana anasema msimu uliopita haukuwa tu sehemu ya mafanikio kwake, bali ulimjengea heshima kubwa kufuatia kuinusuru Junguni na janga la kushuka daraja.
Anasema wakati anatua Junguni kwa mkopo akitokea Mafunzo, aliikuta timu hiyo ikiwa tayari imeshafanya maandalizi ya Ligi Kuu lakini kocha Damian Mussa alimpa nafasi kuonyesha uwezo wake.
“Katika wakati wangu wote wa soka, msimu uliopita ndio bora zaidi kwangu na namshukuru sana mwalimu kwa kuniamini, licha ya kuikuta timu imeshafanya maandalizi, lakini nilipata nafasi,” anasema.
Unapobahatika kupata nafasi ya kukutana na kipa huyo akiwa kitaani kwake ni mtu mtulivu huku mwenyewe akisema muda mwingi huutumia kusikiliza mawaidha ya Kiislamu.
Historia yake ya soka, anasema akiwa mdogo, hakuwa anavutiwa kucheza nafasi ya golikipa ingawa kipaji hicho ni urithi kutoka kwa kaka yake huku yeye akiwa anapenda kucheza nafasi ya beki.
Nyota huyo aliyekulia katika mikono ya Yanga U17, kisha Selem View, Junguni United na sasa Mafunzo, anasimulia kwa tabasamu akisema siku moja alipokuwa mazoezini huku yeye akiwa miongoni mwa wachezaji tegemeo wa nafasi ya beki, ndiyo ilibadilisha kila kitu katika maisha yake ya soka.
Anasema siku hiyo wakati wa mazoezi, kipa mmoja hakufika, hivyo akaamua kuchukua nafasi yake ili ratiba ziendelee, baada ya kumaliza, ndipo mwalimu alivutiwa naye, akaamua kumtumia golini japo yeye hakuridhia.
Baada ya kuanza kutumika kama golikipa kutokana na kocha kuridhika na uwezo wake upande huo, anasema ndipo safari yake mpya ilianzia hapo, huku akimtaja Juma Kaseja ndiye aliyekuwa kioo chake.
Anasema hapo ni nyumbani kwao hataki kuondoka na kuacha alama mbaya kwa sababu ikitokea atahitaji kurudi tena atakuwa huru ingawa anaitumia timu hiyo kama daraja la kupiga hatua moja mbele zaidi ya hapo.
Ameeleza kuwa sababu mojawapo ya kurejea Mafunzo ni kumalizia mkataba wake wa miaka miwili alionao, huku akigusia kuhusu ofa kadhaa alizowahi kuzipata kutoka timu za KVZ, JKU na Mlandege lakini akaamua kuziacha.
Mbali na hilo, anasema anahitaji timu yake ijivunie uwepo wake na yupo tayari kuifanya iendelee kushika nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar.
Anasema hapo awali mpira kwa upande wa Zanzibar ulikuwa unachukuliwa kama starehe, lakini mitazamo imebadilika na kuamini kuwa kwa sasa ni ajira.
Pia, mashabiki wamekuwa na mwamko wa kufika uwanjani kwa wingi tofauti na awali hali inayodhihirisha jambo hilo.
Mbwana anasema unapoamua kuwa golikipa unapaswa kuzingatia kubeba lawama kwa sababu nafasi hiyo ina ugumu ndani yake.
Akitolea mfano, anasema mshambuliaji anaweza kufanya makosa ikaonekana kawaida, lakini kipa akifanya kosa moja linafuta mazuri yake yote.
Lakini hilo kwa upande wake halimuathiri sana kwa vile ameshajipanga kisaikolojia na kulitambua kwani kabla ya mechi anapunguza baadhi ya vitu ambavyo vinaweza kumfanya awe dhaifu uwanjani.
Hata hivyo, Mbwana ameonyesha kusikitishwa na tabia za baadhi ya makocha wanaohusika kuua vipaji vya wachezaji kwa kutowapa nafasi ilhali wana uwezo.
“Walimu wengi wanakosea katika suala la kumuamini mchezaji, wanasahau kuwa wao ndio wenye nafasi ya kumfanya mchezaji kuwa bora na watamfanya mchezaji kuwa dhaifu ikiwa atajengwa kwa maneno mazuri,” anasema.
Anaamini kuwa, endapo makocha watatumia maneno ya kuwatia hofu wachezaji wanapokosea hilo linaathiri vipaji, hivyo ametoa wito kwa viongozi wa nafasi za juu katika mpira kutumia nafasi zao kuwajenga vijana wadogo wenye uwezo na sio kuwapoteza.
Anasema wapo vijana wenye uwezo ambao wakipewa nafasi wanaweza kufanya makubwa hivyo kwa mantiki hiyo wazingatie hilo ili kuongeza ushindani katika Ligi.
Shomari anasema kati ya ndoto ambazo hajazifikia hadi sasa ni kuichezea timu ya Taifa na anamatani kukumbukwa kwa mazuri yake na sio kwa mabaya.
Kipa huyo anamaliza kwa kusema ikifika wakati wa kustaafu anahitaji kuacha alama nzuri ili wengine wajifunze kupitia kwake.