SMARTPIKA YAGAWA MAJIKO YA UMEME SHULE YA MSINGI KIBASILA


Katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha
asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,
kampuni ya Smartpika kupitia Mradi wa Huduma za Kisasa za Upikaji (MECS)
imegawa majiko sanifu ya umeme katika Shule ya Msingi Kibasila jijini Dar es
Salaam, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufikia nyumba milioni tano nchini.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Smartpika,
Andron Mendes, alisema mpango huo unalenga kuwafikia Watanzania milioni 20
ifikapo mwaka 2034, kwa lengo la kuwawezesha kutumia nishati safi ya kupikia
kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uhusiano na Ushirikiano wa
Smartpika, Bobu Yona, alisema kampuni hiyo imejipanga kusaidia kupunguza
gharama za matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia teknolojia rahisi na
rafiki kwa mazingira.

Naye Mwakilishi wa Mradi wa MECS, Charles Barnabas,
alibainisha kuwa matumizi ya majiko sanifu ya umeme ni nafuu zaidi na
yanachangia kupunguza uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi ya kuni
na mkaa.

Akitoa shukrani kwa niaba ya shule, Mwalimu Mkuu wa Shule ya
Msingi Kibasila, Halima Hassan, alisema majiko hayo yamepunguza gharama za
mapishi shuleni pamoja na kulinda afya za wapishi kutokana na kupungua kwa
moshi wa nishati chafu.