TBA kujenga nyumba za makazi, ofisi Pwani

Kibaha, Pwani. Ili kukabiliana na changamoto ya makazi iliyopo mkoa wa Pwani, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), umesema utajenga nyumba za makazi ya watumishi wa Serikali na wananchi, pamoja na ofisi za wawekezaji katika mkoa huo unaosifika kwa wingi wa viwanda.

Imeelezwa Pwani inaviwanda zaidi ya 1650 hivyo kuna wafanyakazi wengi, Wakala huo wa Serikali ulio chini ya Wizara ya Ujenzi utajenga nyumba watakazoishi wafanyakazi hao, watumishi, wafanyabiashara sambamba na ofisi za wawekezaji.

Wakati TBA ikisema hayo, Pwani imeendelea kukua kwa kasi huku wakazi wa Dar es Salaam pia wakitajwa kuufanya mkoa huo mbadala wa makazi yao.

Kwa sasa Dar es Salaam ina watu zaidi ya milioni tano kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 huku wengi wao wakitajwa kukimbilia mkoa wa Pwani wenye wakazi zaidi ya milioni mbili hasa maeneo ya jirani kama Kibaha, Mkuranga na Bagamoyo.

Akizungumzia Mkurugenzi wa Miliki TBA, Said Mndeme leo Ijumaa Oktoba 24, 2025 katika ziara ya ukaguzi wa maeneo yanayomilikiwa na TBA, iliyofanyika mkoani Pwani kwa lengo la kuangalia shughuli zinazohusiana na usimamizi na uendelezaji wa milki za Serikali.

Amesema makazi kwa Pwani imekua changamoto kwa watu huku baadhi yao wakilazimika kuishi mbali na maeneo wanayofanyia kazi.

“Wakala umeona fursa hii na kwa sasa katika mkoa wa Pwani unamiliki nyumba 176, viwanja 535 na changamoto ya makazi TBA inaenda kuishughulikia,” amesema.

“Tutakaa pamoja sisi TBA, Serikali ya mkoa wa Pwani ili maeneo gani tupeleke nguvu ni wapi tukaendeleze nyumba za makazi na ofisi kulingana na uhitaji,” ameongeza.

Katika hilo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema mkoa huo kuna uhitaji wa ujenzi wa ofisi za wawekezaji wakiwemo wa viwanda hata makazi ya watumishi hivyo ni fursa kwa Wakala huo.

Amesema TBA wachangamkie fursa hiyo waone namna ya kupata eneo katika maeneo ya kimkakati ya kiuwekezaji katika mkoa huo huku akisema Pwani ni rahisi kujenga kutokana na uwepo wa viwanda vinavyozalisha miundombinu ya ujenzi.

Amesema mkoani hapo kuna viwanda vya nondo, saruji, marumaru vinapatikana kokoto pamoja na mchanga.

“Tunaviwanda vingi ambapo wafanyakazi wake wanahitaji makazi. Wawekezaji wetu hawana ofisi zilizo karibu na maeneo yao. Hivyo hawana maeneo watakayoweza kufanya ofisi au kuishi. Hii ni fursa kwa TBA,” amesema.

Onyo latolewa kwa wavamia maeneo ya TBA

Aidha, Wakala huo umeonya wale wote wenye tabia ya uvamizi wa maeneo inayomiliki nchini ikisema ni uvunjaji wa sheria.

Wakala huo umesema wote wenye tabia hiyo wakikutwa sheria itachukua mkondo wake huku ikisisitiza wananchi wasiingilie wala kuvamia maeneo hayo inayomiliki.

Katika kusisitiza hilo TBA imesema asithubutu mtu kuingilia eneo linalomilikiwa nalo na endapo akitokea mtu ameshajenga taratibu zitafuatwa na ujenzi huo utaondoshwa.

“Maeneo yote yale ambayo yanamilikiwa na TBA, tayari yamewekewa alama wananchi wasithubutu kuingilia au kuvamia. Tutafata taratibu endapo imebainika umeingilia hata kama kuna maendeleo umeyafanya basi utaondoshwa.

“Nitoe rai wananchi waogope maeneo haya yanayomilikiwa na Serikali kwa maana wakifanya hivyo tutafuata taratibu za kisheria na wataondoshwa,” amesema Mndeme.

Amesema Wakala huo umeshaweka mabango makubwa na alama zenye kuonesha maeneo yote inayomiliki hivyo hawatarajii kuona watu wakivamia maeneo hayo.

Mndeme amesema wakala unaendelea kuhakikisha milki za Serikali zinalindwa vyema ikiwemo kuhakikisha uwepo wa nyaraka stahiki za umiliki yaani hatimiliki, kuweka mabango makubwa yenye jumbe zinazoonesha eneo linamilikiwa na Serikali.

“Kuna wakati unakuta maeneo yetu yana nyaraka zote za umiliki lakini bado baadhi ya watu wanavamia ikiwemo kwa kutokufahamu kama panamilikiwa na Serikali,” amesema.