TBA YAKAGUA VIWANJA 535 MKOA WA PWANI, YAWEKA MKAKATI WA MIRADI YA MAKAZI


Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umefanya ukaguzi wa viwanja 535 vinavyomilikiwa na taasisi hiyo mkoani Pwani kwa lengo la kuvilinda dhidi ya uvamizi na kuviandaa kwa ajili ya uendelezaji wa miradi ya makazi.

Akizungumza leo, Oktoba 24, 2025, wakati wa ukaguzi wa maeneo ya Mwendapole – Kibaha na Kibiki – Chalinze, Mkoani Pwani, Mkurugenzi wa Idara ya Miliki wa TBA, Bw. FRV Said Mndeme, amesema kuwa kwa muda mrefu maeneo hayo hayajatumika ipasavyo, na sasa taasisi hiyo imeanza maandalizi ya kuyapanga na kuyaendeleza.

Bw. Mndeme ameongeza kuwa mpango wa kuanza ujenzi wa nyumba katika viwanja hivyo utasaidia kupunguza changamoto ya makazi kwa wananchi na watumishi wa umma na sekta binafsi mkoani humo.

“Lengo letu ni kuhakikisha miliki za Serikali zinalindwa ipasavyo, nyaraka zinakuwa sahihi, na maeneo haya yanapatiwa hati miliki. Kutokana na ongezeko la mahitaji ya makazi, tumejipanga kuongeza kasi ya uendelezaji wa mali za Serikali mkoani Pwani,” amesema Bw. Mndeme.

Aidha, amebainisha kuwa TBA inamiliki nyumba 176 na viwanja 535 mkoani humo, na tayari wameanza kuweka alama za utambulisho kwenye maeneo yote wanayomiliki nchini ili kulinda dhidi ya uvamizi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, amesema mkoa huo una jumla ya viwanda 1,653, ikiwemo vikubwa 156 na vya kati 190. 

Ameongeza kuwa tangu kuanza kwa Serikali ya Awamu ya Sita, kumekuwa na ongezeko la viwanda vipya 244 ambavyo ni vikubwa vya kati .

Amesema viwanda hivyo vinahitaji makazi na ofisi, huku akisisitiza umuhimu wa kuandaa kikao kazi kati ya serikali ya mkoa na TBA ili kuonesha fursa na mahitaji yaliyopo katika sekta ya makazi na miundombinu.