Udasa yatoa mapendelezo 10, UDSM yajitenga nayo

Dar es Salaam. Wakati Jumuiya ya Wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa) ikitoa mapendekezo takribani 10 ya kufanyiwa kazi na Serikali baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, chuo hicho kimesema hakihusiki na tamko hilo.

Udasa kupitia kwa Mwenyekiti wake, Dk Elgidius Ichumbaki katika taarifa kwa umma iliyotolewa Oktoba 23, 2025, imetaka hatua za haraka kuchukuliwa kukomesha matukio ya utekaji.

Hatua hiyo inalenga ustawi wa vizazi vya sasa na baadaye na kutoruhusu siasa za chuki kuwa chanzo cha uadui kwa Watanzania, ikielezwa Katiba inatamka wazi Tanzania ni nchi ya demokrasia ya vyama vingi.

“Kutokana na mwenendo wa kisiasa unaoendelea nchini, tumeanza kuona chuki za kisiasa zikiongezeka na kusambaa kwa kasi. Kama vyombo vyetu vya usalama havitaweza kulikomesha tatizo hili la utekaji na watu kupotezwa, kuna uwezekano mkubwa wa utekaji kuongezeka,” imeelezwa katika tamko hilo na kuongeza:

“Na hili lisidhaniwe kuwa kati ya upinzani na chama tawala, bali hata ndani ya chama tawala na upinzani pia wakidhuriana wao kwa wao.”

Baada ya tamko la Udasa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, Oktoba 23, 2025, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye, kupitia taarifa kwa umma amesema chuo hicho hakitambui na wala hakihusiki kwa namna yoyote na tamko lililotolewa na Udasa kwani jumuiya hiyo ina uongozi wake na misimamo yake binafsi.

“UDSM inaendelea kuwa taasisi ya umma inayozingatia misingi ya kitaaluma, Katiba na sheria za nchi na maadili ya umma na kujikita kwenye mijadala yenye tija kwa maendeleo endelevu na mshikamano wa kitaifa,” imeeleza taarifa na kuongeza:

“Tunatoa wito kwa Watanzania wote wenye sifa kisheria kushiriki uchaguzi kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 kwa amani, utulivu na uzalendo, tukizingatia kwamba amani ni msingi wa maendeleo na demokrasia na ustawi wa Taifa letu.”

Udasa inapendekeza baada ya uchaguzi mkuu, Bunge lijalo litambue kuwa ni muhimili unaojitegemea na liko kwa ajili ya masilahi ya wananchi, pia vyombo vya ulinzi na usalama na taasisi za dola zijiepushe kutumika kisiasa.

Inapendekezwa kuundwa Tume ya Jaji au Kamati Maalumu ya Bunge kuchunguza matukio ya utekaji na upoteaji wa watu ili haki itendeke kwa waliofanyiwa matendo hayo.

Vilevile, imeshauri makosa yanayohusu uchaguzi yasichukuliwe kama makosa ya jinai, badala yake yawe ya kusahihishwa. Vyombo vya usimamizi wa sheria kama vile Jeshi la Polisi vijiepushe na matumizi makubwa ya nguvu wakati wa kampeni na kupiga kura.

Udasa imesema chama chochote kitakachoshika madaraka kianzishe mchakato wa maridhiano ya kitaifa utakaotokana na utashi wa kisiasa.

Vilevile, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi iwe na uwakilishi wa makundi yote ya kisiasa, kijamii, kidini na asasi za kiraia.

Imeshauri baada ya wajumbe wa tume kupatikana, wao ndio wamchague Mwenyekiti wa Tume atakayeapishwa na Jaji Mkuu, badala ya kuteuliwa na Rais ambaye naye pia ni mgombea kwenye uchaguzi.

“Vyombo vya habari visinyimwe uhuru wa kutoa taarifa zinazohusu kasoro za uchaguzi wanazoziona kwa ushahidi wa wazi,” inapendekezwa.

Udasa imesema vyombo vya habari viruhusiwe kuwa sehemu ya kupigania na kusimamia uwazi katika mchakato wa uchaguzi na kama kuna upungufu visaidie kuuibua na mamlaka husika ziweze kuurekebisha.

Jumuiya hiyo imesema ni muhimu kuhakikisha uwepo wa uwazi wakati wa kuandikisha wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura na hata wakati wa kuhesabu na kujumlisha kura, ili zoezi zima la uchaguzi liwe la kuaminika kwa Watanzania na kuonyesha dunia kuwa michakato  ya uchaguzi ni ya kidemokrasia.

Jumuiya hiyo imesema viongozi walio na kinga ya kisheria wajizuie kudharau Katiba ikieleza Katiba ndiyo sheria mama au sheria namba moja ambayo kila Mtanzania lazima aheshimu na kuifuata.

“Wanasiasa wasijione wao pekee ndio wenye haki zote kuhusu michakato ya kidemokrasia nchini. Haki ya kuchagua na kuchaguliwa ni ya Watanzania wote na uamuzi wa mustakabali wa kisiasa uwe mikononi mwa Watanzania,” imeeleza taarifa ya Udasa.