Unguja. Wakati kampeni za uchaguzi mkuu zikielekea ukingoni, vyama vya siasa vimeeleza namna vilivyoendesha kampeni na mipango ya siku za lala salama kuhakikisha vinaibuka kidedea.
Hata hivyo, licha ya kuhakikisha vinakamilisha kampeni, vimeeleza changamoto kubwa viliyokutana nayo kuwa ni ukata, uliosababisha vishindwe kufanya mikutano mingi ya hadhara.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kampeni zilizozinduliwa Septemba 11, 2025 zitafungwa Oktoba 27, 2028 saa 12:00 jioni kipisha kura ya mapema itakayopigwa Oktoba 28 kabla ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Licha ya ratiba hiyo ya ZEC, hakuna chama hata kimoja kati ya 11, kilichosimamisha wagombea wa kiti cha urais na kuzindua kampeni zake Septemba 11, 2025. Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT- Wazalendo, vilizindua kampeni Septemba 13, 2025 vyama vingine vilitumia wiki moja au zaidi kuanza kampeni.
Moja ya changamoto kubwa ni ukata ambao unatajwa kuvikumba vyama vingi na kujikongoja kuwafikia wananchi, licha ya udogo wa eneo la Zanzibar.
Hata hivyo, pamoja changamoto hiyo vyama hivyo vimefanya kampeni angalau mara moja kwa wiki, kuhakikisha vinaeleza sera zake.
Mwananchi limezungumza na baadhi ya mameneja kampeni wa vyama hivyo na kueleza namna ambavyo vimeendesha kampeni zake “za kisayansi” na jinsi wanavyojipanga kumalizia ngwe iliyobaki kabla ya Uchaguzi Mkuu Jumatano Oktoba 29, 2025.
Meneja wa kampeni na uchaguzi wa NCCR Mageuzi, Nadir Nyoni amesema licha ya kutofanya kampeni za mikutano mingi ya hadhara, wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuendesha kampeni za nyumba kwa nyumba na kuwafikia watu wengi zaidi.
“Mtu anaweza kuona hatupo sana kwenye majukwaa lakini tumetembelea wananchi mmoja mmoja kwenye mitaa kuhakikisha tunafikisha ujumbe wetu na kuomba kura,” amesema Nyoni.
Katika vyama 11 vilivyopitishwa na ZEC kuwania urais Zanzibar, NCCR Mageuzi ndicho kilichochelewa zaidi kuzindua kampeni zake hadi Oktoba 3, 2025.
Tangu kilipozindua kampeni hizo kimefanya mikutano mitatu ya hadhara.
Katika hilo Nyoni amesema ni kutokana na uwezo ni mdogo kifedha kwa kuwa mkutano mmoja mdogo unagharimu zaidi ya Sh2 milioni.
Hata hivyo, amesema katika kampeni walizofanya kupita kwa watu, wananchi wameonyesha kuwapokea na kuwakubali kutokana na kuwa ni mwanamke, hivyo wanaamini wataweza kufanya vizuri katika uchazui huo.
“Tusiwe waongo watu wanatupokea vizuri lakini kwenye kufanya uamuzi huwezi kujua maana wanabadilika, lakini wengi wamehamasika hasa walipoona tumemsimamisha mgombea wa kike,” amesema Nyoni.
Anasema hawakutegemea kupata mwitikio kama walioupata na kwamba bado wanaendela kusaka kura kabla ya mkutano wao wa mwisho utakaofanyika hivi karibuni.
Naye Katibu Mwenezi wa Chama Makini, Fahmi Abdallah amesema wametembelea makundi yote muhimu yakiwemo ya bodaboda, bajaji, wajasiriamali, wafanyabaishara na makundi maalumu.
Amesema badala ya kusubiri wananchi wawafuate kwenye viwanja vya mikutano, wao wamekuwa wakiwafuata kwenye maeneo yao wakiwa wanaendelea na shughuli zao za kujiingiza kipato.
“Kwa kiasi kikubwa tumefikia makundi yote na kwa sasa tumeanza kuyafikia makundi maalumu wakiwemo wajane, watu wenye ulemavu na watoto yatima na tumepata mwelekeo na mapokeo mazuri katika makundi yote,” amesema.
Amesema wameamua kutumia mbinu hiyo ili kuwafikia walengwa wenyewe na kutokana na rasimali fedha ndogo waliyonayo, kwa kuwa hawakuweza kufanya mikutano mikubwa.
Kwa upande wake, Meneja wa kampeni wa AAFP, Omar Juma Said amesema pamoja na changamoto zilizojitokeza, wanashukuru wamefanikiwa kuendesha kampeni zao na kuyafikia makundi na wananchi wengi kwenye maeneo yao.
Amesema katika mikutano yao waliyofanya wamepata mapokeo makubwa na wananchi kukubali sera zao na kuwa wamekuwa wakipata ushirikiano wa ZEC na Polisi kuhakikisha mikutano yao inalindwa bila kupata vurugu.
“Kwa jicho la kawaida zaidi ya asilimia 70 tumefanikiwa na tumeyafikia makundi ya kura, wakati tukieleka mwisho kuna baadhi ya mikutano tutafanya kuhakikisha makundi yote yanafikiwa bila kuacha hata moja,” amesema.
Amesema katika kuliendeea hilo mwishoni wanataka kuwafikia zaidi vijana kwani ndio wapigakura wengi.
Pamoja na hayo amesema katika mikutano yao ya mwisho watahakikisha wanapata wakarimani wa lugha, kwani wameona kuna umuhimu maana kuna baadhi ya maeneo wameenda na kukutana na changamoto hiyo na kuwakosesha haki ya kusikiliza sera zao.
