Wadau wavishauri jambo vyombo vya usalama kutumia utu kulinda amani

Kahama. Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imetumia kauli ya ‘Kazi na Utu’ kuvishauri vyombo vya usalama kutumia utu katika kuimarisha amani iliyopo nchini badala ya kutumia nguvu na kuzua taharuki na hasira miongoni mwa jamii.

Mjumbe wa JMAT Kahama, Kagoma Kasagamba, akizungumza kwa niaba ya mwenyekiti wa jumuiya hiyo leo Oktoba 24, 2025, Sheikh Amir Hassan amesema endapo vyombo vya usalama vitatumia nguvu dhidi ya wananchi wasio na silaha zozote, vinaweza kuivuruga amani iliyopo.

Ameyasema hayo leo Oktoba 24, 2025 wakati akitoa tamko la JMAT Kahama kuhusu uwepo wa tetesi za maandamano zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii, yanayosemekana kufanyika siku ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, Oktoba 29, 2025.

Amevikumbusha vyombo vya usalama kutowaficha watu wanaoshikiliwa kwa sababu za kiusalama, badala yake wajulikane walipo ili kuepuka kupandikiza hasira kwa wananchi ambao hata hivyo haoni kama kutakuwa na maandamano na JMAT haiungi mkono suala hilo.

Kasagamba ambaye pia ni makamu askofu wa Kanisa la FPCT Jimbo la Kahama, amesema “Hawa watu hawana silaha, hawana chombo, inapotumika nguvu kubwa kuwadhibiti inakuwa ni hatari, itumike nguvu ya wastani.”

Ameongeza: “Watu wasifichwe, wajulikane walipo, tumemchukua huyu kwa ajili ya usalama, yupo sehemu fulani na ikiwezekana aonekane, ukimficha mtu ni kama kuwawasha moto wa hasira, lakini ni ukweli kabisa kwamba tunawahimiza watu kujitokeza kupiga kura kutumia haki zao za kikatiba.”

Aidha, JMAT imetoa tamko la kutounga mkono fujo za aina yoyote zitakazosababisha nchi kukosa amani huku akiwaasa Watanzania kujiepushe na mambo yanayoweza kuipoteza amani iliyopo nchini, huku akieleza kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.

Amesema: “Hatuungi mkono, fujo ya aina yoyote itakayosababisha nchi hii kukosa amani, lakini tunashauri watu wawe na subra, haki ipo tu hatakama itacheleweshwa, itatokea tu baada ya uchaguzi Tanzania ipo na na maisha bado yataendelea.

“Watu wengi wanadhani amani ipo kwa sababu kuna haki, amani inakuwepo kwa sababu ya mambo mawili ikiwemo haki na uvumilivu, kuwepo kwa amani hata kama haki haipo. Inawezekana kabisa haki haipo lakini ukaangalia kama utadai haki kwa nguvu kupita kiasi, kuna hatari ukakosa haki na amani ikavurugika.”

Ameshauri kila Mtanzania mwenye sifa za kupiga kura kujitokeza ili kumchagua kiongozi anayemfaa sambamba na kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika kuepuka misuguano na vyombo vya usalama.

Kijana kutoka Wilaya ya Kahama, Alan Salvatory amesema: “Mimi nitakachofanya siku hiyo ni kupigakura, habari ya maandamano hapana, kwa sababu maisha yangu bado najitafuta, nina familia inanitazama leo hii amani ikikosekana familia yangu itakuwaje? Watanzania tuwe wapole kama ni haki tudai kwa utaratibu.”

Naye Safina Salumu, mkazi wa Mhongolo amesema: “Naona tu kwenye mitandao kuwa kuna kuandamana kudai haki, sasa utumike utaratibu mzuri wa kudai maana unapozungumzia maandamano tutasema na kudai haki lakini inawezekana kabisa yakawa chanzo cha machafuko nchini.”