Wakulima wagawiwa mashine za umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji

Dodoma. Serikali imegawa mashine 250 za umwagiliaji zenye thamani ya Sh3.3 bilioni kwa wakulima 2,264 wanaotoka kwenye mikoa saba yenye uhakika vya vyanzo vya maji ikiwa ni awamu ya kwanza ya mradi wa majaribio kwa kipindi cha miezi sita ili kuongeza uzalishaji wa mazao hasa ya mbogamboga na matunda.

Mikoa itakayonufaika na mradi huo wa majaribio ni Ruvuma, Tanga, Mwanza, Simiyu, Mara, Kagera na Geita ambapo jumla ya wilaya 16, vijiji 93 na wakulima 2,264 wanaomiliki hekari takribani 4,000 watanufaika na mradi huo.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Oktoba 24, 2025 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye viwanja vya maonyesho ya wakulima, Dk John Samweli Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.

Mweli amesema hiyo ni awamu ya kwanza ya kugawa miundombinu ya umwagiliaji kwa wakulima nchini ambapo wameanza na mikoa hiyo saba kwa kipindi cha miezi sita na baada ya hapo kutakuwa na awamu nyingine zitakazofuata ili kuwafikia wakulima wote nchini.

“Tulifanya tathmini nchi nzima ili kuona mahitaji ya wakulima ambapo katika awamu hii ya kwanza tumeanza na mikoa saba ya Ruvuma, Tanga, Mwanza, Simiyu, Mara, Kagera na Geita na katika mikoa hiyo saba tunaanza na Wilaya 16 ambayo ina vijiji 93 na wakulima 2,264 ambao tayari wameshabainishwa huku hekari zitakazomwagiliwa ni takribani 4,000,” amesema Mweli na kuongeza kuwa:

“Lengo letu ni tuachane sasa na masuala ya misimu kwa sababu misimu ni kukosa mvua, sasa hivi tunapokwenda wakati miradi mikubwa ikiendelea kukamilika na inaendelea na ujenzi hawa wakulima wetu waliopo kwenye vyanzo vya maji tunawapatia miundo mbinu sasa ya kuweza kulima mwaka mzima kama vile matunda mboga mboga na mazao mbalimbali.”

Mweli amesema kwenye ajenda ya 10/30 malengo ni kuhakikisha kuwa kilimo kinafikia asilimia 10 kwa mwaka ifikapo mwaka 2030 ambapo kati ya maeneo muhimu ya kufikia malengo hayo ni eneo la umwagiliaji ambalo limegawanyika katika maeneo mawili.

Amesema eneo la kwanza ni miradi mkubwa ya umwagiliaji ambayo ipo 780 ambapo humo ndani kuna miradi ya uchambuzi yakinifu ya kujenga mabwawa makubwa na miradi mikubwa ya umwagiliaji nchi nzima.

‎Ametaja eneo la pili kuwa ni la umwagiliaji mdogo mdogo kwa ajili ya wakulima wadogo walioko ngazi ya mikoa na ambao wapo karibu na vyanzo vya maji karibu na mito mikubwa ambao wanatumia maji ya mito kwa uchache na siyo kwa ufanisi na wale ambao wana visima.

‎Amesema katika awamu hii ya kwanza ya mradi inajumuisha uchimbaji wa visima, usimikaji wa miundombinu midogo ya kumwagilia ikiwemo umwagiliaji wa matone pamoja na miundombinu ya unyunyiziaji ambapo pia mkulima atapatiwa pampu ambayo ina uwezo wa kuvuta maji hadi mita 500 kutoka kwenye chanzo cha maji, mpira wenye urefu wa mita 500 na chombo cha umwagiliaji ambacho ni springler (mashine ya unyunyiziaji).

Katika amwamu hii ya kwanza wataanza na visima 500 ambavyo vitawekwa miundombinu ya kuhifadhi maji na wanatarajia mradi huo uwaguse wanawake na vijana ambao wanajishughilisha na kilimo cha mbogamboga na matunda nchini.

Amesema wakulima watakaonufaika na mradi huu ni wale ambao wapo kwenye vikundi vya kuanzia watu 10 hadi 30 ambapo kwenye kikundi cha watu 10 watapewa mashine moja ya umwagiliaji na walioko kwenye kikundi cha watu 30 watapewa mashine tatu zenye uwezo wa kumwagilia hekari moja kwa saa.

Mratibu wa programu ya uhimilivu wa mifumo ya chakula kutoka Wizara ya Kilimo, Timotheo Semguluka amesema wizara kwa kushirikiana na watafiti wanafanya utafiti wa udongo na kuupima kwa lengo la kutengeneza ramani ya udongo ambayo itatoa picha na maelekezo sahihi kuanzia ngazi ya kijiji ambapo mkulima atajua afya ya udongo wa shamba lake, aina ya mbolea atakazotumia ili kuongeza tija.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Agrova ambaye ndiye msambazaji wa mashine hizo za umwagiliaji, Kwilasa Kakila amesema kampuni hiyo inashirikiana na benki ya kilimo ya TCB kukopesha mashine hizo kwa wakulima ambao hawana uwezo wa kununua pamoja na benki nyingine ikiwemo benki ya Ushirika.