Watu wasiojulikana wachoma nyumba ya Polisi Songwe

Songwe. Watu wasiojulikana wamechoma moto nyumba ya Polisi Kata wa Chitete iliyopo Kijiji cha Ikumbilo, Wilaya ya Ileje mkoani Songwe. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea usiku wa Oktoba 22, 2025 wakati askari huyo akiwa kwenye majukumu maalumu.

Kamanda Senga amesema nyumba hiyo inamilikiwa na Mkaguzi wa Polisi, Nsajigwa Mwajeka ambaye ni polisi kata wa eneo hilo, na kwamba moto huo uliunguza vitu kadhaa kwenye vyumba viwili na uligunduliwa na Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Darkson Kamendu. 

Amevitaja vitu vilivyoteketea katika nyumba hiyo kuwa ni pamoja na nguo za kiraia, sare za polisi, vyombo kadhaa, mahindi, kitanda, godoro na vitu vingine vidogo, vyote vikiwa na thamani ya takribani Sh2 milioni. 

“Chanzo cha tukio bado kinachunguzwa, lakini inaonyesha wahalifu walikusanya vitu na kuviweka kitandani kisha kuchoma moto kwa kutumia njiti za kiberiti zilizokutwa eneo la tukio,” amesema Kamanda Senga. 

Hata hivyo, Kamanda Senga amesema hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa, japo kuna watu wanaendelea kufuatiliwa na pindi watakapokamatwa, jeshi hilo litatoa taarifa kamili.