Wazawa waipa Mlandege ushindi wa kwanza Ligi Kuu Zanzibar

BAADA ya bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Zanzibar, Mlandege kuanza kwa kusota msimu wa 2025-2026, hatimaye imetoa gundu kwa kupata ushindi wa kwanza kwa kuifunga New Stone mabao 3-0, kikosi kikiwa na wachezaji wazawa pekee.

Mechi hiyo ilichezwa Oktoba 22, 2025 kwenye Uwanja wa Gombani uliopo kisiwani Pemba saa 10:15 jioni ambapo wafungaji wa mabao hayo ni Omary Ramadhan ‘Babatov’ na Mussa Hassan ‘Mbappe’ aliyefunga mawili.

Hadi kufika sasa timu hiyo ina jumla ya pointi sita katika mechi tano huku ikishinda moja pekee, sare tatu na kupoteza moja.

Kikosi cha Mlandege chenye mchanganyiko wa wachezaji wa kigeni na wazawa, katika mechi dhidi ya New Stone, ilitumia wazawa pekee jambo lililoonekana kuwashangaza mashabiki na kuwa na maswali mengi juu ya wachezaji wakigeni kutocheza kwani haijazoeleka.

MLA 01

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Msaidizi wa Mlandege, Sabri China amesema  wamefurahishwa na ushindi huo huku akisema sababu za kuchezesha wazawa pekee ni baadhi ya wachezaji kupata majeraha katika mechi zilizopita, hivyo wamewapata mapumziko.

Pia, amesema wameamini uwezo wa wachezaji wazawa walionao ndio maana wakaamua kuwachezesha kwa kuangalia kiwango chao ili kupambana na changamoto za ligi hiyo.

Amesema, kikosi hicho kinatarajiwa kushuka tena Dimba la Gombani kuivaa Fufuni na mkakati wao ni kuondoka na alama sita kisiwani humo.

Vilevile, amesema ushindi huo ni mwanzo mzuri wa safari ya Mlandege katika kutetea ubingwa wa ZPL msimu huu.

Wachezaji wa kimataifa waliopo Mlandege ni Vitor De Souza na Davi Nascimento (Brazil), Hamis M’sa na Alphonce Ahmed (Comoro), Fortune Chidera (Nigeria), Ishamel Robino (Ghana) na Enzo Claude (Ufaransa).

MLA 02

Ukiachana na Mlandege, timu ya Chipukizi nayo imefungua ukurasa mpya wa kupata bao la kwanza tangu msimu uanze na Massoud Chudi ndiye mfungaji wa kwanza aliyeifungulia ukurasa huo timu hiyo baada ya jana Oktoba 23, 2025 kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Uhamiaji kwenye Uwanja wa Mao B, Unguja.

Kabla ya hapo, Chipukizi ilipokea vipigo vitatu ambavyo ni; KVZ 1-0 Chipukizi, Mwembe Makumbi 2-0 na Malindi 1-0 Chipukizi, sare zikiwa pia tatu, haijaonja ushindi. Nyavu zake zimetikiswa mara tano.

Junguni United nayo haikuwa nyuma, imevuna mabao mawili baada ya kuilazimisha sare Mwembe Makumbi ya mabao 2-2, katika mechi iliyochezwa jana Oktoba 23, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A uliopo Unguja.

Wakati timu tatu zikitoa gundu ZPL, New Stone iliyopanda daraja msimu huu bado haina bao wala alama ikishuka dimbani mara tano, ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 15.