Kampuni ya mawasiliano ya Yas imeonesha tena dhamira yake katika kuendeleza michezo na utalii nchini baada ya kushiriki kwenye uzinduzi rasmi wa maandalizi ya Kilimanjaro International Marathon 2026.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam ukihudhuriwa na wadau mbalimbali wa michezo, wakiwemo waandaaji wa mbio hizo, wadhamini na wanariadha, huku Yas ikithibitisha kuendelea kudhamini mbio za nusu marathon (km 21) kwa mwaka wa 11 mfululizo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Yas, Christina Murimi, alisema kampuni hiyo imejenga urafiki wa kudumu na mashindano hayo kutokana na mchango wake mkubwa katika kuhamasisha afya, utalii na maendeleo ya kijamii.
“Kwa niaba ya Yas na Mixx, tunajivunia kuwa sehemu ya tukio hili muhimu ambalo limekuwa likiwaleta pamoja Watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali. Ushirikiano huu si wa biashara tu, bali ni jitihada za dhati za kuunga mkono jamii kwa njia endelevu,” alisema Bi. Murimi.
Kwa mujibu wa Murimi, kampuni hiyo imekuwa ikitumia teknolojia za kisasa za 4G na 5G kuhakikisha washiriki na watazamaji wanabaki kuunganishwa wakati wote wa tukio hilo. Aidha, kupitia huduma za Mixx, washiriki na wadhamini wanapata urahisi wa kufanya malipo kwa njia za kidijitali kwa usalama na ufanisi mkubwa.
“Kwa kutumia nguvu ya teknolojia, tunahakikisha kila hatua unayoipiga kwenye mbio hizi ni yenye tija. Hii ndiyo njia yetu ya kuleta mageuzi chanya katika michezo na jamii kwa ujumla,” aliongeza.
Kwa upande wake, kamati ya maandalizi ya Kilimanjaro International Marathon imeeleza kuwa maandalizi ya mwaka 2026 yameanza mapema zaidi kuliko kawaida ili kutoa nafasi kwa washiriki kujipanga vizuri.
Usajili unatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni, huku wanariadha kutoka mataifa mbalimbali wakitarajiwa kujiunga.
Tangu kuanzishwa kwake zaidi ya miaka kumi iliyopita, Kilimanjaro Marathon imekuwa sehemu ya kuunganisha jamii, kukuza utalii na kuchochea uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro na taifa kwa ujumla.
