Aga Khan kuchunguza bure saratani ya matiti kila Jumamosi

Dar es Salaam. Madaktari bingwa wa saratani nchini wametoa wito kwa Watanzania, hasa wanawake, kujichunguza mara kwa mara ili kubaini mapema dalili za saratani ya matiti, wakisisitiza kuwa ugonjwa huo unatibika endapo utagundulika mapema.

Saratani ya matiti kwa sasa inashika nafasi ya pili kwa wingi wa wanaougua saratani nchini, baada ya mlango wa kizazi na inachangia asilimia 30 ya wagonjwa wote wa saratani wanaopokelewa kila mwaka katika Hospitali ya Aga Khan.

Wito huo umetolewa leo Oktoba 25, 2025, katika tukio la matembezi maalumu ya uhamasishaji kuhusu saratani ya matiti, jijini Dar es Salaam, likihusisha wadau wa afya kutoka sekta binafsi na umma.

Matembezi hayo yamebeba ujumbe wa vita dhidi ya saratani ya matiti si ya mtu mmoja, bali inahitaji nguvu ya pamoja kutoka kwa Serikali, sekta binafsi na jamii.

Akizungumza baada ya matembezi hayo, daktari bingwa wa magonjwa ya saratani wa hospitali hiyo, Harrison Chuwa amesema saratani ya matiti kwao ni ya kwanza ambapo huona wagonjwa wapya 250 hadi 300, sawa na asilimia 30 ya wagonjwa wote ikiwa na maana kuwa wanagundua wagonjwa wapya 100 kwa mwaka.

“Kinachotia wasiwasi ni ongezeko la wagonjwa vijana, wenye umri wa kati ya miaka 30 hadi 40 ambapo zamani tulizoea ugonjwa huo ni kwa watu wenye miaka 40 na kuendelea,” amesema Dk Chuwa.

Wadau mbalimbali wa afya wameshiriki katika matembezi maalumu ya uhamasishaji kuhusu saratani ya matiti yaliyoandaliwa na Hospitali ya Aga Khan

Amesema kuna haja ya kufanyika tafiti ili kujua kuna mabadiliko gani kwa saratani kutokana na umri mdogo wa wagonjwa wakati awali ilikuwa kwa watu wazima.

Dk Chuwa amesema lengo kuu la kampeni hiyo ni kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa mapema.

“Saratani ikigundulika mapema, inatibika, tunataka watu waelewe kuwa uchunguzi si wa mwezi wa Oktoba pekee. Usisubiri Oktoba unaweza kufanya uchunguzi mwezi wowote, iwe Desemba au Machi. Hiyo ndiyo zawadi bora ya maisha yako,” amesema.

Amesema Hospitali ya Aga Khan imeanzisha huduma ya bure ya uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti kila Jumamosi, ambapo wagonjwa watakaobainika kuwa na dalili wataelekezwa Taasisi ya Ocean Road kwa matibabu zaidi.

“Uchunguzi huu ni bure, na kwa wale watakaohitaji vipimo vya ziada kama mammogram ambayo ni X-ray ya matiti  kutakuwa na punguzo la asilimia 50. Hii ni njia ya kusaidia wanawake wengi zaidi kujitokeza.”

Ameongeza kuwa kila baada ya miezi mitatu, Aga Khan itakuwa ikiendesha matukio kama hayo kwa saratani tofauti, ili kuendeleza elimu kwa jamii.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Dk Bryceson Kiwelu amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika huduma za matibabu ya saratani, huku sekta ya umma na binafsi zikishirikiana kwa karibu kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Tunamshukuru Mungu kwa kuwa sasa nchi yetu imefika mahali ambapo sekta binafsi na ya umma zinashirikiana kwa karibu kuhakikisha ujumbe sahihi unafika kwa jamii kwa wakati sahihi,” amesema Dk Kiwelu.

Amesema huduma za matibabu ya saratani sasa zinapatikana kwa ubora wa hali ya juu katika vituo mbalimbali nchini, ikiwemo Ocean Road, KCMC, Bugando, Mbeya, na hospitali za mikoa, huku pia sekta binafsi kama Aga Khan ikichukua jukumu la kuelimisha na kutoa huduma za uchunguzi wa awali.

Kuhusu wanawake kujichunguza, Dk Kiwelu, amewataka wawaelimishe wenzao na hata waume zao au wapenzi wao, kuwasaidia kutambua mabadiliko yoyote yasiyo ya kawaida.

“Unapokuwa unaoga au unapomaliza kuoga, jitazame, jipapase matiti yako. Kwa sababu ni mwili wako, utajua kama kuna mabadiliko, ukiona kitu kisicho cha kawaida, nenda kituo cha afya mara moja. Tumeshuhudia wagonjwa wakitibiwa na kupona, matibabu yapo na ni ya uhakika,” amesema Dk Kiwelu.

Kiongozi wa Mradi  mtambuka wa saratani kwa wanawake nchi za Afrika Mashariki, Dk SaraJennifer Maongezi amesema wamepata ufadhili wa euro milioni 110.2 sawa na Sh228 bilioni kwa ajili ya malengo makuu matatu ambayo ni kuimarisha huduma za uchunguzi na tiba ya saratani, kufanya tafiti za kiafya, na kujengea uwezo wahudumu wa afya na jamii.

“Tafiti zitajikita zaidi kwa wanawake, hasa wale wanaokabiliwa na saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti.